Karoti ni moja kati ya mazao ya mbogamboga yenye thamani kubwa hivi sasa hapa nchini. Kilimo chake huhitaji uangalizi mdogo, hivyo hata mtu ambaye ana majukumu mbalimbali anaweza kumudu. Karoti ni zao kutoka jamii ya mzizi na ina vyanzo vingi vya Calcium, Iron na Vitamin B. Karoti inahitaji udongo wenye PH 5.5-6.8, udongo wa kichanga na laini ambao unaruhusu hewa na maji kupita.
Kwa Tanzania, zao hili linalimwa kwa wingi katika mikoa ya Mbeya, Morogoro (Uluguru na Mgeta), Iringa, Kilimanjaro na Kagera. Karoti inastawi katika hali joto la wastani kuanzia nyuzi joto 15 hadi 20 japokuwa inaweza kustahimili katika nyuzi joto 27. Soko la karoti ni la uhakika kwa sababu inatumika kama kiungo katika vyakula mbalimbali.
Karoti zinazolimwa kwa wingi Tanzania:
- Nantes: Aina hii inapatikana maeneo mengi na inalimwa sana hapa Tanzania. Ukuaji wake ni wa haraka
- Chantenay Red Core: Ladha ya karoti hii ni nzuri na inataka kufanana na Nantes lakini mizizi yake ni dhaifu ukilinganisha na ile ya Nantes.
- Oxheart: Karoti za Oxheart ni fupi na nene. Huvunwa baada ya muda mfupi kulinganisha na aina nyingine.
Karoti hupandwa kwa kutumia mbegu moja kwa moja shambani bila kupandikiza. Kiasi cha mbegu kinachotumika kupanda ni kilo 3.5 mpaka 4 kwa ekari. Mstari mmoja hadi mwingine ni sentimita 30 na mche mmoja hadi mwingine ni sentimita 10. Hii inaweza kubadilika kulingana na aina ya karoti. Baada ya wiki ya nne kutoka kupandwa, inatakiwa kung’olea miche iliyorundikana ili kuipa nafasi.
Mkulima anatakiwa kuhakikisha kuwa udongo una unyevu muda wote. Kama sio kipindi cha mvua, anashauriwa kumwagilia angalau mara mbili au mara tatu kwa wiki ili udongo uwe na unyevu wa kutosha. Karoti inapokosa maji ya kutosha huzalisha mizizi midogo ambayo ni dhaifu, na udongo mkavu unapopata maji mengi kwa wakati mmoja, husababisha karoti kupasuka.
Wadudu:
- Minyoo Fundo: Minyoo hii hushambulia mizizi na kuipelekea kuwa na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na hivyo kupunguza mavuno. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao ya jamii ya karoti. Vilevile, hakikisha shamba ni safi muda wote.
- Imi wa Karoti: Mashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Tumia dawa kama Dichlorvos, Sapa Diazinon na Fenvalerate.
- Karoti kuwa na mizizi mingi (Folking): Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Sababu nyingine ni matumizi ya mbolea za asili ambazo hazijaoza vizuri.
Kulingana na hali ya hewa, karoti huvunwa baada ya miezi mitatu au kuanzia wiki 11 hadi 13. Karoti huvunwa kwa kung’oa miche na kuchukua mizizi yake. Endapo mkulima atalima kwa kuzingatia ushauri wa watalaamu, mavuno ya zao hili kwa ekari moja ni kuanzia tani 10 hadi 15.