Home BIASHARA Unatumia njia sahihi kujitangaza?

Unatumia njia sahihi kujitangaza?

0 comment 93 views

Ili kufanya biashara na kupata matokeo mazuri inabidi ujitangaze ili watu wajue kuhusu bidhaa au huduma unayotoa. Tangazo ni moja ya njia ambazo humvutia mteja kutumia bidhaa au huduma husika inayotangazwa, hivyo ubunifu ni muhimu wakati wa  kutengeneza tangazo kuhusu biashara yako.

Sawa unaweza kutangaza biashara yako bila kutumia gharama yoyote lakini unatakiwa kujua kuwa haitokuwa rahisi na juhudi kubwa sana inahitajika ili kuwavutia watu kuja kununua au kutumia bidhaa au huduma unayotoa. Hivyo ni muhimu kwa mfanyabiashara kutenga bajeti kwa ajili ya matangazo hii itamsaidia kufanya shughuli nyingine huku wateja wakiendelea kununua bidhaa au  huduma husika.

Kuna njia mbalimbali za kutangaza biashara, njia hizo ni kama; kutangaza biashara kwa njia ya mdomo (hii hutumika zaidi baina ya marafiki, familia), kutangaza biashara katika vyombo vya habari kama televisheni, redio, magazeti, kutangaza biashara katika tovuti au blog za watu, kutangaza kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Whatsapp n.k.

Njia zote ni nzuri lakini mfanyabiashara anatakiwa kutafakari njia ambayo inafaa kutangaza biashara yake. Kitendo cha kujua aina ya wateja wanaokuja kununua bidhaa au kuja kutumia huduma unayotoa ni jambo la kwanza litakalokusaidia kujua ni katika mfumo gani unatakiwa kuelekeza fedha zaidi ya matangazo. Kwamfano siku izi watu wa rika wanatumia zaidi mitandao ya kijamii kuliko kusikiliza radio au televisheni au hata kusoma magazeti hivyo hakutakuwa na maana wewe kulipia tangazo la laki mbili kwenye gazeti ukiwa unatangaza nguo au viatu vya kisasa vya watu wa rika.

Hivyo ni vyema kwenda na wakati, na vile vile kuangalia huduma au bidhaa unayouza imelenga watu wa mtindo gani. Ikiwa huna bajeti ya kutosha mbali na kutumia njia kama mitandao ya kijamii, tovuti nk unaweza kutumia fursa zifuatazo kuitangaza biashara yako kwa gharama nafuu kwa mfano kwa kuhudhuria semina na makongamano yanayohusu biashara hasa zinazoendana na biashara yako mara nyingi katika makongamano hayo huwa kunakuwepo waku wa rika tofauti hivyo kwa kujichanganya unaweza kujipatia wateja wa aina mbalimbali.

Misaada, ni namna moja wapo ya kupata wateja wapya katika biashara yako. Hapa si lazima uwe na fedha ili uweze kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji. Unaweza kuandaa operesheni ya kukusanya nguo zisizotumika lakini zina hali nzuri kwa watu mbalimbali hasa wa karibu baada ya hapo unazisafisha na kuziweka katika hali nzuri na kwenda kuzigawa kwa watu wenye uhitaji, picha yako moja tu inayoelezea shughuli hiyo inaweza kubadilisha muelekeo wa biashara yako na masuala ya kifedha kwa ujumla kwani siku zote watu huvutiwa na matendo madogo. Ndio maana tunaona kila siku makampuni makubwa yanatoa misaada mbalimbali na yanatangazwa katika vyombo vya habari hiyo ni moja ya njia ya kujitangaza.

Mbali na hayo siku zote watu hupenda kupewa ushauri wa bure kuhusu mambo mbalimbali. hivyo ikiwa unauza bidhaa au huduma fulani na ukawa unapenda kufafanua mambo mbalimbali kuhusu huduma au  bidhaa husika basi utajipatia wateja wengi kwa sababu kwanza wateja wataona unawajali na kupata hamasa ya kutumia huduma au bidhaa hiyo kutokana na mirejesho kutoka kwa watu wengine walifuata ushauri wako. Kwa mfano kama unauza bidhaa ya nywele jitahidi kuwaelimisha wateja kuhusu aina ya nywele, aina ya mafuta ya kutumia kulingana na nywele; hii itamvutia mteja kununua bidhaa yako kwa sababu atakuwa amepata uelewa kabla ya kununua bidhaa hiyo.

ili kujua zaidi kuhusu matangazo na njia sahihi ya kutangaza biashara ni muhimu ukijisomea vitabu au makala zinazohusu mambo ya matangazo ili kupata ufahamu zaidi na kufanya maamuzi yatakayoleta maendeleo zaidi katika biashara yako.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter