Home BIASHARA Ushauri kwa biashara za rejareja

Ushauri kwa biashara za rejareja

0 comment 107 views

Ujasiriamali ni jambo zuri, na watu wengi hutafuta fedha ili waweze kujiajiri ili kupata maendeleo makubwa zaidi. Biashara za rejareja huchangamkiwa na watu wengi kwa sababu hazihitaji mamilioni kuanzisha. Mara nyingi wafanyabiashara wa bidhaa za rejareja huweka bidhaa mbalimbali ili kuwahamasisha watu kununua bidhaa hizo.

Ieleweke kuwa, hakuna mafanikio ambayo hupatikana kwa urahisi, kuna watu wamefanikiwa kupitia biashara za rejareja lakini haimaanishi kuwa walipata mafanikio hayo kirahisi. Hivyo ikiwa unataka kuanzisha biashara ya rejareja au umeshaianzisha tayari, basi jitahidi kuzingatia haya ili kupata mafanikio zaidi:

Jambo la muhimu sana katika biashara yoyote hususani ya rejareja ni eneo. Unaweza kuwa na bidhaa nzuri na duka la kuvutia lakini kutokuwa na wateja ni changamoto kubwa kwa sababu lengo la kufungua biashara husika ni kujipatia wateja na kunufaika, kukosa wateja maana yake hakuna biashara. Hivyo ikiwa unaanza biashara yako hakikisha kuwa eneo lako ni rahisi kufika, na wakazi wa eneo hilo wana uhitaji wa bidhaa unazouza. Usifungue biashara katika sehemu ambayo inakidhi mambo yako binafsi.

Kuna kitu kinaitwa ‘theme au motto’ ni muhimu pia katika biashara ya rejareja. Ndio maana katika maeneo mengi utasikia ‘nenda kwa mangi kaninunulie kitu fulani’ kwa sababu mtumaji anakuwa na uhakika kuwa kitu hiko kipo. Hivyo hakikisha unakuwa na utambulisho wako, kwa mfano kama unataka kuuza bidhaa za kike kwanza unaweza kuanza na jina la biashara yako, unda jina linaloendana na bidhaa unazouza ili kuwapa wateja urahisi ikiwa wanahitaji bidhaa fulani. Utambulisho wako ni muhimu kwani unaweza kukupatia wateja wengi zaidi.

Kwenda na wakati ni muhimu katika biashara. Urahisi wa kwenda na wakati hutokana na maoni ya wateja. Hivyo ni muhimu kusikiliza maoni ya wateja, kusoma vitabu, makala, kuangalia televisheni, kupitia mitandao ya kijamii n.k ili kupata habari mpya hususani kuhusu bidhaa unazouza au zinazoendana na bidhaa zako. Kwenda na wakati si vibaya kwanikwa kufanya hivyo, unajipatia wateja wengi zaidi, lakini kuwa makini na bajeti yako, usinunue bidhaa nje ya bajeti ili tu kwenda na wakati, hakikisha unatengeneza mpango mathubuti ikiwa ni pamoja na kwenda kwenye duka la jumla kuangalia bidhaa mpya  zilizopo na zitakazoletwa ili kujua kama unaweza kumudu kununua bidhaa hizo na kupata faida zaidi au la.

Wafanyakazi. Ikiwa utaajiri watu katika biashara yako kuwa makini. Biashara nyingi zinakosa wateja kwa sababu ya mienendo ya wafanyakazi. Ukiwa unataka kuajiri mtu jitahidi kujua mambo kuhusu mtu unayemuajiri ikiwa ni pamoja na kuuliza sehemu ambazo amewahi kufanya, kujua mambo anayopendelea kufanya na muhimu zaidi kumpa sheria na kanuni za kazi ili iwe rahisi kuchukua hatua ikiwa atafanya kazi kinyume na inavyotakiwa.

Punguzo la bei (Sale). Wateja wengi hufurahia neno hili kwa sababu watu hupata vitu wanavyovitaka au kuvitamani kwa fedha sawa na bure. Hivyo ili kuwahamasisha wateja kufika au kukuungisha bidhaa zako si vibaya kuwa na punguzo kila baada ya muda, hii itakusaidia kuuza bidhaa zilizokaa muda mrefu, kuleta mzigo mpya, kujipatia wateja wapya, na kupata wateja wa muda mrefu.

Kwa ujumla biashara zina changamoto na mazuri yake. Fanya utafiti wa kutosha kabla ya kufanya maamuzi ambayo aidha yanaweza kukunufaisha au kukuletea hasara. Sio lazima kuwekeza moja kwa moja katika biashara kwani si kila mtu anaweza kuwa mfanyabiashara. Unaweza kuangalia fursa zilizopo ikiwa unaweza kuzifanyia kazi wewe mwenyewe basi fanya, ikiwa unaona kuna mtu mwingine anaweza kutelekeza fursa hiyo zaidi yako basi wekeza kwa mtu huyo, lengo ni kupata maendeleo.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter