Siku zote wafanyabiashara hushauriwa kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kufungua biashara zao. Kwa kufanya utafiti inakuwa rahisi kufanya maamuzi sahihi. Ni muhimu kufuatilia mambo yote kwasababu jambo lolote utakalopuuzia linaweza kukuletea shida siku za mbeleni na kupelekea kuifunga biashara yako.
Matumizi ya fedha ni moja ya masuala muhimu katika biashara. Lengo la biashara ni kupata faida na si vinginevyo, lakini ili kuanzisha biashara mfanyabiashara hutakiwa kutumia fedha nyingi ili kuhakikisha biashara yake ipo katika hali nzuri. Hivyo baada ya kutumia fedha nyingi kuanzisha biashara mmiliki anatakiwa kutengeneza mahusiano mazuri na watu kwa mfano wauzaji (suppliers) ili kurahisisha majadiliano ya kupunguza bei ya manunuzi ya mzigo, bei ya usafirishaji, nk.
Muda mwingine mmiliki anatakiwa kutumia fedha nyingi zaidi ili kuongeza mapato zaidi. Hivyo ni muhimu kutafakari kwa kina maamuzi yako kuhusu matumizi ya fedha. Kwa mfano ili kuitangaza biashara yako unatakiwa kutumia fedha, hivyo fikiria matokeo unayoweza kupata kwa kutumia fedha kutafuta wateja. Ukipata jibu itakuwa rahisi kufanya maamuzi na kupata matokeo stahiki.
Suala la eneo la biashara pia linaweza kuwa linakusababishia utumie fedha nyingi ya kodi. Siku hizi wafanyabiashara wanatumia mitandao zaidi kuuza bidhaa zao hivyo angalia wapi unauza bidhaa zaidi, kama watu wachache wanafika ofisini kwako basi unaweza kufikiria kuihamishia biashara yako nyumbani na kuboresha zaidi uuzaji wa bidhaa mitandaoni ikiwa ni pamoja na kuweka bajeti kwaajili ya kuitangaza biashara yako.
Wafanyabiashara wanashauriwa kuajiri wafanyakazi kwaajili ya kazi maalumu. Ili wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii mmiliki anatakiwa kuwalipa mshahara mzuri wafanyakazi na kuhakikisha wanapata faida mbalimbali, lakini kama unatumia fedha nyingi kwaajili ya wafanyakazi si vibaya ukiwaajiri wafanyakazi muda na kuachana na wafanyakazi wa moja kwa moja (fulltime). Ni rahisi kuwalipa wafanyakazi wa muda mfupi kwa sababu wafanyakazi hao hulipwa kwa masaa na kazi waliyoifanya na si kila mwezi au wiki inategemeana na makubaliano yaliyopo baina ya muajiri na muajiriwa.
Usafiri ni moja ya mambo ambayo yanaweza kuwa yanatumia fedha nyingi katika biashara yako hivyo angalia kiasi cha fedha unachotumia kwaajili ya usafiri halafu tafuta njia mbadala ili kutumia fedha kidogo kwa mfano kama unatumia gari inayotumia mafuta mengi unaweza kuiuza gari hiyo na kununua gari inayotumia mafuta machache.
Kuwa mmiliki wa biashara kuna majukumu mengi sana na kunahitaji umakini hivyo mmiliki anashauriwa kutilia maanani kila jambo linalotokea katika biashara yake ili kuepusha matatizo kutokea na ikiwa yametokea kutafuta suluhisho kabla tatizo halijawa kubwa