Wajasiriamali wengi wamekuwa wakihoji umuhimu wa kusoma elimu ya juu baada ya kuanzisha biashara zao. Asilimia kubwa husisitiza kuwa kuanzisha biashara ilikuwa ni funzo kubwa kuliko elimu inayotolewa vyuoni. Japokuwa hii inaweza kuwa kweli, elimu ya chuo bado ni nguzo muhimu kwa wajasiriamali. Kufanikiwa darasani na katika biashara kuna uhusiano mkubwa kuliko watu wanavyofikiria.
Elimu ya chuo humhakikishia mjasiriamali nguzo hizi muhimu na zenye mchango mkubwa katika sekta ya biashara.
- Maarifa
Chuo ni sehemu ambayo kuna fursa mbalimbali. Uwepo na matamasha, watu wa aina mbalimbali, mikutano n.k ni nafasi za kipekee kwa wanafunzi. Kama ukitumia vizuri fursa hizo, ushauri pamoja na maarifa ambayo hutolewa yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika maisha yako ya ujasiriamali. Tumia nafasi hii kujenga mahusiano ja watu sahihi ambao watakusaidia hapo baadae.
- Umakini
Mara nyingi wajasiriamali wanashindwa sio kwa sababu wanakosa maarifa yanayotakiwa bali ni kutokana na kushindwa kuwa makini na kukosa mbinu sahihi za kutumiza malengo yao. Chuo ni sehemu pekee ambayo inampa mtu uwezo kwa kuwa makini katika maamuzi yake hivyo unapoanzisha biashara pasipo kuwa na maarifa haya kuna uwezekano mkubwa kuwa utashindwa kuimudu siku za mbele.
- Upana wa mawazo
Kuna aina mbalimbali za watu chuoni na hiyo hupelekea mtu kuwa na mawazo ya iana mbalimbali kutokana na aina ya watu anaokutana nao. Uwepo huu wa aina tofauti ya watu hufanya chuo kuwa sehemu ya maarifa na mawazo ya kila aina. Uwezo wa kusikiliza na kukabiliana na mawazo kutoka kwa watu mbalimbali ni msingi muhimu katika biashara yoyote. Chuo ni sehemu muhimu ya kujifunza kuishi na watu tofauti.
- Uwezo wa kujenga mahusiano
Uwezo wa kutengeneza mahusiano na watu maana yake ni kwamba upo katika nafasi nzuri ya kukubalika katika jamii. Hii husaidia kuishi vizuri na watu wa aina mbalimbali nah ii inamaanisha kuwa ukiwa na biashara yako, unaweza kufanya kazi na kila mtu. Uwezo na kuwasiliana na kutengeneza mahusiano ya muda mrefu chuoni humuandaa vyema mjasiriamali kukabiliana na watu tofauti baadae. Hakuna biashara bila mahusiano mazuri na watu.
- Nidhamu ya muda
Katika biashara, nidhamu ya muda ni mojawapo ya vitu ambavyo humsaidia sana mtu kitimiza malengo yake. Hii ni sawa na chuo kwani ukiwa mwanafunzi wa elimu ya juu hakuna mtu atakayekupa maagizo ya nini cha kufanya hivyo nidhamu yako katika kutekeleza majukumu ndiyo chachu ya maendeleo yako. Kuwa na uwezo na kupangilia majukumu na kuheshimu muda wako na wa watu wengine ni muhimu sana katika biashara.
Elimu bado ina mchango mkubwa katika maisha yetu hata kama umefanikiwa katika biashara. Vijana ambao wanajipanga kujiajiri na kuingia rasmi katika sekta ya ujasiriamali wanatakiwa kutambua mchango wa elimu katika mafanikio ya biashara ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi pale muda wa kujiajiri unapofika.