Ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kuhakikisha kuwa wateja wote wanapata huduma stahiki na kuondoka wakiwa wameridhika. Lakini hiyo haitakiwi kuwa sababu ya mfanyabiashara kusahau malengo yake wakati akijaribu kumridhisha kila mtu kwani biashara inaweza kuathirika kwa namna moja au nyingine.
Biashara huanzishwa kwa lengo la kusaidia au kuwarahisishia watumiaji. Kama mfanyabiashara unatakiwa kujua kuwa huwezi hata siku moja kuwaridhisha wateja wa aina zote hivyo badala ya kuhangaika kuweka kila aina ya bidhaa au huduma jitahidi kulenga katika upande ambao unaweza kumudu kwa sababu hata ukiweza kukidhi mahitaji ya kila mtu, lazima kutakuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu. Ili kurahisisha na kuhakikisha malengo ya biashara yanatimia ni muhimu kujihusisha na kundi maalumu la watu/watumiaji kwa kuwa itakuwa rahisi kuwahudumia na kuhakikisha wanapata huduma au bidhaa wanazotaka.
Ni kawaida kwa wateja kutoa mapendekezo katika huduma au bidhaa unayouza. Ni jambo zuri kumsikiliza kila mteja lakini wewe kama mfanyabiashara unatakiwa kuangalia ni mapendekezo gani unaweza kuyafanyia kazi na yapi yapo nje ya uwezo wako. Kwa kuwa na mfumo huo itakurahisishia kupata wateja wa kudumu kwa sababu kwa kusema ‘hapana au ndio’ na kutoa sababu kutamuwezesha mteja kuelewa kwanini kile kitu anachotaka hakitaweza kufanyiwa marekebisho hivyo itamfanya aelewe kuwa hata kama akija tena, anaweza kukuta mabadiliko au la. Lakini kusema ndio katika kila mapendekezo na kushindwa kutekeleza kutawafanya wateja waone kuwa hujali mawazo yao na inaweza kuwapelekea kwenda sehemu nyingine ambayo wanaweza kusikilizwa na kupata huduma wanayoitaka.
Kumridhisha kila mtu kunaweza kuwachanganya hata wateja kwani hata wakati wa kutengeneza matangazo unashindwa kujua aina husika ya wateja, hali ambayo itakulazimu kutengeneza matangazo ya aina mbalimbali ili kuwafikia wateja wote. Lakini kuwa na aina husika ya wateja inaleta urahisi kuwafikia na vilevile kujitangaza.
Kwa ujumla,kuwa mmiliki wa biashara inamaanisha kuwa unayo mamlaka ya kusema ndio au hapana ili kulinda maslahi ya biashara yako. Hivyo basi, hakikisha umelenga kundi fulani na ikiwa wateja wana mapendekezo basi fanyia kazi mapendekezo yaliyo ndani ya uwezo wako na kwa yale yasiyowezekana basi jitahidi kueleza kwanini haiwezekani na kupendekeza njia mbadala.