Tanzania imetakiwa kuwekeza kwa haraka katika elimu na afya za watu wake hasa vijana kama itataka kuimarisha rasilimali watu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Kauli hiyo imo katika toleo jipya la jarida la Uchumi la Benki ya Dunia.
Imeelezwa kuwa katika miaka ya karibuni Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya binadamu ambapo imeweza kupunguza idadi ya vifo kwa watoto chini ya miaka mitano, kuongeza miaka ya wanafunzi kuwa shule kwa vijana wake na kuimarisha umri wa uhai kwa watu wazima.
Hata hivyo takwimu za urari wa uzalishaji wa binadamu yaani Human Capital Index (HCI) ya 0.40 inamaananisha kuwa watoto wanaozaliwa leo nchini Tanzania wanaweza kufikia asilimia 40 tu ya pato wanaloweza kulipata wakiwa na afya njema na elimu.
“Utajiri nchini Tanzania umeongezeka kwa asilimia 45 toka mwaka 1995 na haya ni mafanikio makubwa, lakini pia idadi ya watu imeendelea kuongezeka, na hivyo kupungua kwa pato halisi na hivyo kukosa uendelevu,” anasema Bella Bird, Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Tanzania.
“Ili nchi iwe na ukuaji endelevu, inahitaji kuwekeza kwa watu wake, kwani raslimali watu ni muhimu sana kwa nchi yoyote ile.”
Benki ya Dunia ilizindua HCI Oktoba 2018, kama mradi mpya wa kushawishi mataifa kuwekeza zaidi kwa wananchi wake.
Urari huo unaangalia vipengele vitano vyenye kuonesha kipato cha baadae: uhai wa watoto baada ya miaka mitano; Wastani wa miaka inayokamilishwa na vijana kujipatia elimu; Ubora wa elimu katika shule;ni kwa miaka mingapi watu watafanyakazi, kama kipimo cha uhai wa mtu mzima utapitiliza miaka 60 na kuzuia udumavu kwa vijana na watoto.
“Kuna mambo mengi kwa Tanzania na mataifa mengine kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa katika urari huo ( HCI ) nchi za Singapore, Korea Kusini, Japan, na Hong Kong.
Mataifa haya mafanikio yake yameelezwa kutokana na kuwekeza zaidi katika vijana, wakizingatia zaidi elimu na maendeleo ya utaalamu katika ngazi zote za makuzi yao,” anasema Quentin Wodon, Mchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia na Mwandishi mwenza wa toleo la 12 la uchumi wa Tanzania.
Kwa kuangalia kiwango chake cha maendeleo, Tanzania haifanyi vyema miaka ya kijana kuwa shuleni na kuna hatari ya watoto chini ya miaka 5 kudumaa.
Ripoti zinaonesha pia urari mbaya wa mapato kijinsia inakwamisha kuongeza ubora wa raslimali watu na hivyo pato la utajiri.
Ili kukabiliana na vikwazo vinavyozuia maendeleo ya raslimali watu, serikali imeshauriwa kuimarisha uwekezaji katika maeneo mengi kwa kutumia nguvu yake yote na kutoa huduma bora.
Pia mkazo umetakiwa kuwekwa kwa makundi yenye shaka hasa wasichana wanaokua na kwa kuangalia maeneo ambayo yapo nyuma.
Pia wametaka muda wa wanawake kufanya kazi wasizolipwa kama utunzaji wa familia upunguzwe, kwa kusambaza wajibu huo ili kuwawezesha kufanya kazi zaidi zinazowalipa.
Pia kuwapa nafasi zaidi wanawake kumiliki mali za kufanyia uzalishaji, kuangalia hali ya soko na mifumo ya kitaasisi inazuia fursa kwa wanawake.
Jarida hilo la sasa linaloelezea hali za uchumi pia limetoa maoteo ya hali ya uchumi kwa miaka michache ijayo. Kuangalia changamoto za mazingira ya nje ya biashara na uwekezaji kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku ikitambulika kwamba kwa Tanzania hali inakuwa bora zaidi.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema ukuaji huo utategemea utekelezaji wa mabadiliko katika sera.
Pia hatua za serikali kuboresha mazingira biashara na kifedha ikiwamo kupunguza tozo, kurejesha fedha kwa wananchi hasa za kodi na kuweka kipaumbele kwa miradi ya uwekezaji inayolenga kuleta maendeleo na yenye fedha tayari za kumalizia miradi kwa wakati uliopangwa.