Home BIASHARA Kila muuza furniture anahitaji vitu hivi

Kila muuza furniture anahitaji vitu hivi

0 comment 396 views

Kila mtu anahitaji samani (furniture) nzuri nyumbani kwake, na hata ofisini. Hii haimaanishi kuwa kila kampuni ya furniture hutengeneza bidhaa zinazowaridhisha wateja wote.

Nini cha kufanya ili kuweza kufanikiwa katika biashara hii?

Sio rahisi kwa kila kampuni kutumia njia moja ili kupata mafanikio lakini kuna baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kufanyika ili kufanikiwa. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na thamani ya bidhaa zinazotengenezwa na huduma bora kwa wateja.

Ili kutengeneza bidhaa zenye ubora ni muhimu kwanza kuelewa jamii ambayo inakuzunguka. Ni vyema kujua mahitaji yao. Hii itakurahisishia kujua bidhaa zako zinatakiwa kuwa katika mtindo gani, itakurahisishia kupanga bei na kuitangaza biashara yako.

Yafuatayo ni mambo muhimu ambayo kila biashara ya furniture inapaswa kuzingatia:

Huduma bora

Mara nyingi wateja hulalamikia huduma mbovu, hivyo hakikisha kila mteja anapata huduma bora inayozidi matarajio yake. Huduma bora humfanya mteja kumuamini mfanyabiashara na kampuni kwa ujumla. Hakikisha unawasiliana na wateja wako mara kwa mara na ni muhimu kuepuka kutoa ahadi ambazo huwezi kutekeleza.

Timu yenye uzoefu

Timu yako inaweza kusababisha bidhaa yako ichukuliwe namna fulani, hivyo hakikisha timu yako hasa ya mauzo inaelewa kila kitu na ina uzoefu wa kutosha ili kurahisisha mazungumzo baina yao na wateja. Mara nyingi wateja huwa hawajui nini hasa wanahitaji hivyo ni muhimu kuwa na timu ambayo inaweza kuwasaidia wateja kupata kile wanachokitaka. Kila mfanyabiashara anatakiwa kujua kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na timu bora,

Viwango na ubora

Wakati matangazo yatawafanya watu kufika katika eneo lako la biashara, ni muhimu kuwa na bidhaa zenye viwango na ubora wa hali ya juu ili kuwavutia wateja. Jitahidi kupanga samani zako katika hali ya kuvutia na pia jifunze kutokana na malalamiko ya wateja kwa kuboresha bidhaa zako. Aidha, endelea kuwa mbunifu na weka kitu kipya mara kwa mara.

Soko

Si rahisi kutengeneza bidhaa kwa ajili ya kila mtu. Hili jambo lisilowezekana na linaweza kukuchanganya kwa kiasi kikubwa na mwishoni kusababisha biashara isiendelee. Fahamu unataka wateja wa aina gani na wekeza nguvu kubwa katika matangazo. Siku hizi kuna wauzaji mbalimbali wa furniture kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kwamba hii ni njia rahisa ya kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.

Bei

Baada ya kufahamu walengwa wa biashara yako, inakuwa rahisi kupanga bei ambayo inaendana na kundi hilo. Weka bei kulingana na eneo, walengwa na hali ya soko. Bei yako inayo nafasi kubwa katika kushawishi wateja kuamua kununua hivyo hakikisha gharama ya bidhaa zako ni rafiki. Pamoja na hayo, hakikisha wafanyakazi wanaopeleka bidhaa (delivery)  wana heshima, ni wataalamu na wanazingatia muda.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter