Mtu yoyote huwa na furaha pale anapopata taarifa kwamba anatakiwa kwenda kwa ajili ya usaili wa kazi kwenye ofisi ambayo aliomba kuajiriwa. Maandalizi huwa ni muhimu ili uweze kuipata kazi hiyo. Idadi ya maswali hutegemeana lakini kuna maswali ambayo kila kampuni au taasisi lazima waulize. Watu wengi wamekuwa wakijibu maswali hayo tofauti na vile inavyotakiwa hasa wale ambao inakuwa mara yao ya kwanza.
Haya ni maswali 7 ambayo huulizwa mara kwa mara wakati wa usaili
- Wewe ni nani?
Hili swali watu wengi huona ni rahisi lakini ni kiuhalisia, lina ugumu wake hasa pale unapojibu bila kufikira kwa kina. Mtu anayekufanyia usaili lazima akuulize swali hili, hivyo basi ili kulijibu inavyofaa: kwanza usielezee masuala yako binafsi, anza kwa kueleza kuhusu elimu uliyonayo, historia yako ya kazi, jinsi ulivyoanza, mafanikio ambayo umeyapata hadi ulipofikia na mambo ambayo unatarajia kuyafanya hapo mbeleni na jinsi kazi hiyo itakavyokufikisha unapotaka kufika. Eleza kwa ufupi tu, usitumie muda mrefu kujielezea.
- Kwanini uajiriwe?
Ili kujibu swali hili ipasavyo, unashauriwa kufanya utafiti (research) kabla ya siku ya usaili kuhusu kampuni au taasisi hiyo. Wakati unajibu swali hili ongelea namna ambazo ujuzi ulionao utakavyoleta mabadiliko. Zungumzia mambo maalumu ambayo wakikuajiri utaweza kuyafanya na kuwasaidia.
- Swali kwa muajiri.
Ni vizuri kuuliza swali unapokuwa kwenye usaili. Hii itaonyesha uelewa na pia ni ishara ya kwamba umejipanga na unataka kazi hiyo. Unaweza kuuliza kuhusu muelekeo wa kampuni, kama kutakuwa na mafunzo, uliza kuhusu changamoto ambazo unaweza kuzipata ukiwa umeajiriwa hapo, utakuwa unaripoti kwa nani na kadhalika. Jitahidi kuuliza maswali yanayohusiana na kazi tu.
- Unategemea mshahara kiasi gani?
Hili ni swali tata na linaweza kukusababisha upate mshahara mdogo au hata ukakosa kazi kwa sababu kampuni au taasisi hiyo haiwezi kumudu kukulipa kiasi ulichotaja. Usikurupuke, mwambie msaili kuwa hujafikiria kuhusu kiasi, hauna uhakika na kiasi ambacho wanaweza kukulipa. Sema unahitaji muda kidogo kabla ya kutoa jibu. Kwa mfano, unaweza kusema sasa unachojali ni kupata kwanza hiyo kazi, suala la malipo litafuata baadae ambapo wewe na kampuni hiyo mtajadili na kufikia muafaka.
- Kwanini umeomba nafasi hii?
Hapa unaweza kuelezea jambo maalumu ambalo limekuvutia kuomba nafasi hiyo. Unaweza kuelezea kuhusu huduma, au bidhaa zinazopatikana mahai hapo. Onyesha kwamba kupitia kampuni hiyo, unaona jinsi gani ujuzi wako utaongezeka.
Usiseme hujui kwanini umeomba kazi hiyo, usiseme huna kazi na upo tayari kufanya yoyote ile ndio maana umeomba, usiseme unahitaji fedha. Jitahidi kujibu kama msomi na epuka sababu binafsi ambazo hazitamuonyesha muajiri faida za kukuajiri.
- Umejuaje kuhusu nafasi hii?
Mara nyingi hili huwa ni swali jepesi, unaweza kusema ulisikia kuhusu nafasi hiyo kutoka kwa rafiki, mtandaoni au unawafuatilia sana hivyo huwa unaona taarifa zao mara kwa mara katika mitandao ya kijamii na kadhalika.
- Unafahamu nini kuhusu kampuni?
Msaili anataka kufahamu kama umefanya utafiti wa aina yoyote kuhusu wao pamoja na huduma wanazotoa. Ni vizuri kufanya utafiti wa kina kuhusu kampuni kwa ujumla, huduma au bidhaa wanazojihusisha nazo, wapinzani wao, masoko yao na wateja wao kabla ya kwenda kwenye usaili. Kuwa na taarifa muhimu za kampuni hiyo.
Wakati wa usaili, ni muhimu kutoonyesha uoga. Hakikisha unavaa nguo ambayo itakufanya ujisikie vizuri, jiamini, usisahau kubeba vyeti muhimu na sikiliza maswali yote kwa umakini kabla ya kujibu.