Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Aida Khenani ameihoji serikali kuhusu hatma ya ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu, kufuatia serikali ya awamu ya tano kutotoa ajira kwa vijana tangu mwaka 2015. Khenani amesema hayo wakati akichangia mjadala wa utekelezaji wa kazi za serikali na mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka ujao wa fedha.
“Upatikanaji wa ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu kwa sasa ni tatizo kubwa katika nchi yetu, serikali itueleze hapa bungeni kwanini haiajiri vijana wetu. Nina ujumbe kutoka kwa vijana wengi ambao wanataka tuiulize serikali ni lini itatoa ajira kwao”. Amesema Khenani.
Naye Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango Malecela (CCM) amepongezwa na Spika wa bunge, Job Ndungai baada ya kuchangia mada hio, kwa kueleza kuwa Tanzania inashika nafasi ya 22 duniani kwa uzalishaji wa pamba hivyo ingefaa kama serikali itawekeza zaidi katika zao hilo ili kufufua viwanda vya nguo nchini na vilevile kujenga vipya. Kwa upande wake, Mbunge wa Kaliua Magdalena Sakaya (CUF), ameunga mkono mawazo aliyowasilisha Mbunge Malecela, na kuipongeza serikali kwa kuboresha huduma za kibingwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili (MNH) na taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).