Kama ilivyo katika kazi nyingine, msimamizi mzuri wa mitandao ya kijamii anatakiwa kuwa na ujuzi mbalimbali ili kuwezesha mitandao anayosimamia kupata mrejesho chanya kutoka kwa wafuatiliaji.
Ikiwa unataka kufanya kazi hii lakini hauna uhakika kama utafanikiwa, basi kupitia makala hii utajifunza ujuzi mbalimbali ambao unatakiwa kuwa nao ili kuweza kuifanya kazi hii ipasavyo.
Kitu cha kwanza unachotakiwa kuwa makini nacho ni zile habari unazoweka katika mitandao ya kijamii. Tambua kuwa kila kila applicationhuitaji mtindo tofauti wa uandishi. Kwa mfano kwenye mtandao wa kijamii wa LinkedIn habari zinatakiwa kuwekwa kitaaluma zaidi kuliko kwenye mtandao wa Facebook kwasababu LinkedIn ni mtandao unaohusu mambo ya kazi, wataalamu mbalimbali makini. Hakikisha unaweka vichwa vya habari vifupi lakini vya kuvutia, pia hakikisha maneno unayoandika ni rahisi kwa mtu kusoma kwa sababu wasomaji watakuwa makini na kila kitu kilichoandikwa ikiwemo nukuu, vidokezo vya maelezo na hata takwimu.
Msimamizi wa mitandao anatakiwa kwenda na wakati na kufanya utafiti kila wakati ili kuhakikisha anakwenda sawa na mabadiliko ya kasi yanayotokea kila wakati duniani. Baadhi ya mambo ya kuzingatia ili kwenda na wakati ni pamoja na Hashtags (#) zinazotumika zaidi kutokana na muda, pia matangazo mapya yanayojitokeza kila wakati ni vema kuyatilia maanani ili kuhakikisha hupitwi na mambo yanayotokea, na kujua mambo ambayo washindani wanajihusisha nayo ili kwenda nao sawa na hata kufanya vizuri zaidi yao.
Ujuzi wa SEO ni muhimu ili kuweza kupata wafuatiliaji wengi, kupata idadi kubwa ya watu wanaotembelea akaunti na mwisho wa siku kunufaika kwa kupata fedha kutokana na matangazo kutoka kwa kampuni na biashara mbalimbali. Hivyo kama msimamizi ni vema kuwa na ujuzi kuhusu SEO ili kunufaika mtandaoni.
Kama unataka kufanya kazi na kampuni kubwa ni muhimu kuwa na utaalamu kuhusu mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kujua habari zinazovutia zaidi watu, na ni jukwaa lipi linafaa kuweka habari zipi, pia kuwa na uwezo wa kushawishi wafuatiliaji kuwa wanapitia ukurasa au akaunti yako mara kwa mara.
Huduma kwa wateja katika kazi hii ni muhimu kwa sababu wewe ni kioo cha kampuni au biashara husika. mara nyingi wateja hutizama akaunti za biashara katika mitandao ya kijamii na kuuliza maswali au kutaka kupata maelekezo zaidi, kama hakuna mtu wa kujibu maswali au kuelezea maelekezo zaidi wateja huchukulia biashara husika haiku makini, kitu ambacho si kizuri kwa biashara.
Kuwa tayari kukabiliana na mabadiliko ni muhimu ili kuweza kuendelea kujitangaza. Hivyo kama msimamizi wa mitandao ya kijamii unatakiwa kuhakikisha matukio unayoweka yanaenda sambamba na mabadiliko yoyote yanayojitokeza. Vilevile si vibaya kujaribu mambo mapya ili kujua vitu ambavyo vinawavutia zaidi wafuatiliaji katika mitandao ya kijamii