108
Miongoni mwetu tunatumia asilimia 75 ya muda wetu kwa siku katika kazi.
Kwahiyo kuwa katika kazi ambayo haikupi faraja inaweza ikakuletea matatizo katika maisha yako ya kila siku.
Umejaribu njia zote kujitahidi kuendana na hali lakini bado unaona wazi kabisa kwamba kuna kitu kinakosekana.
Ni ukweli usiopingika kuwa kazi yoyote ile kwa upande mwingine kuna kipindi inachosha.Unachopaswa kujiuliza ni je, hali hii unayojisikia ni ya muda au ni ya kudumu?
Kama ushawahi kukumbana na hali hiyo au kujiuliza hilo swali basi makala hii inakuhusu.Sasa utajuaje kama kazi uliyopo sasa ulifanya uamuzi sahihi kuifanya au ulikosea?
Zifuatazo ni dalili ambazo unapaswa kuziangalia ili kufahamu na kutatua fumbo hili:
1.HUNA SHAUKU YA KUPANDA DARAJA:
Kama upo katika kazi unayoipenda kupanda daraja kwako kitakuwa kipaumbele chako cha kwanza kwani ndicho kitakuwa kipimo cha utendaji wako.Hivyo hicho ni kitu utakachokuwa unapenda kikutokee.Kila mfanyakazi hutegemea baada ya kazi apate ujira wake na kuonyesha uwezo wake katika kazi yake.
Lakini endapo haujawahi kujisikia hali ya kuonyesha uwezo wako ili kupata daraja jipya basi ujue hiyo si hali ya kawaida kuiacha kama ilivyo.
2.UNAJIONA UKO PEKE YAKO:
Kuwa mfanyakazi si kwenda eneo la kazi, kukaa katika meza yako, kufanya kazi yako na kurudi nyumbani.
Ni kushirikiana na kila mtu aliye eneo lako la kazi, kuchangamana nao, kujadiliana masuala ya kazi, nakutumiana katika kujipima uwezo wa kila mmoja wenu.ikikosekana hali hii eneo la kazi hupoteza ladha ya kukalika.
Ikiwa umewahi kufanya juhudi za kuanza kuchangamana na kushirikiana na wenzako lakini imeshindikana mpaka leo.Unapaswa ujiulize ni kwanini hali hiyo inatokea.Inawezekana wenzako wanapishana kabisa na wewe kuanzia malengo mpaka sifa.
3.KILA WAKATI HUISHI KULALAMIKA
Hakuna kazi inayohakikisha kumfurahisha kila anayeifanya kila wakati.
Na lazima katika mabaya yote unakutana nayo lazima kuna machache mazuri yatakuwepo.
Lakini ukijikuta kila kitu unakilalamikia hakuna zuri unaloliona si kitu cha kukiachia hata kidogo,
lazima kutakuwa na tatizo kwako.
Kaa chini uitafakari kazi yako kisha jaribu kuangalia yapi unayaona zaidi mabaya au mazuri,
na endapo mabaya yakiwa mengi basi hiyo ni dalili tosha kwamba unapaswa utafute ustaarabu mwengine.
4.KIPAUMBELE CHAKO NI PESA TU:
Kama ulikuwa hujui pesa inaweza kukuridhisha kwa miezi kadhaa lakini ikishaisha kuridhika kutaegemea zaidi uhusiano wako na kazi unayofanya.
Pesa ni muhimu hilo kila mtu analitambua,
lakini hakutakuwa na thamani hata kidogo kufanya kazi usiyoipenda eti kwa kufuata pesa.
5.HAKUNA JIPYA UNALOJIFUNZA:
Katika kila kazi anayofanya mtu lazima kuna vitu vipya utakuwa unajifunza, na endapo unataka kuongeza uwezo wako wa kufanya kazi ili kupata uzoefu zaidi hiki pia kitakuwa kipaumbele chako.
Soko la ajira linakuwa siku hadi siku na hivyo hitaji la watu wenye uzoefu wa mambo mengi watakuwa hitaji namba moja.
Kama hauna tabia ya kujifunza vitu vipya katika kazi yako basi upo katika hatari kubwa sana ya kupitwa na wakati.Haina maana kujisifu umekaa miaka mingi katika kazi yako lakini huna jipya ulilojifunza.
6.HUJIONI KUKUA KATIKA KAZI YAKO:
Katika maisha kukua ni sifa mojawapo katika jambo lolote unalojihusisha nalo.Hautaweza kuipenda kazi ambayo huoni dalili yoyote ya wewe kukua katika siku zijazo.Kama kilele unachotaka kufikia hakiko wazi kwako,sioni ni jinsi gani utaweka juhudi kukifikia.Kitu hiki hakitaishia kukunyima raha tu, bali kitachukua pia uwezo wako wa kujiamini.Utaanza kuvurugikiwa na hasa hali itakuwa mbaya pale utakapo kuwa unakutana na watu ambao wamefanikiwa katika kazi zao.
7.HAUIONEI FAHARI KAZI YAKO:
Hata kwa kiasi gani ujitahidi kujiambia mwenyewe kuwa kazi unayofanya ni nzuri lakini hauna uthubutu wa kuitaja mbele ya wenzako.Hivi itawezekana vipi mtu uone aibu kuielezea kazi yako mbele ya wenzako halafu uwe unaipenda?
8.UNAJIHUSISHA NA VITU VYA OVYO UKIWA KAZINI:
Kama unafanya kazi unayoipenda utakuwa unakwepa sana kukutana na mambo ya ovyo.Muda mwingi utakuwa unawekeza nguvu yako katika kazi unayofanya na si kujihusisha na vitu visivyohusiana na kazi yako.
Endapo unapenda zaidi kukatisha kazi unayofanya ili kushabikia kitu cha ovyo kabisa hiyo ni dalili tosha hiyo kazi ujiulize tena.
9.HAUTUMII UWEZO WAKO:
Kazi nzuri ni ile inayokupa nafasi ya kujitumia uwezo wako kwa kiasi kikubwa.Kama kazi unayojihusisha nayo haikupi nafasi ya kuonyesha uwezo wako wote basi anza kujitafakari kama ulipo ulipaswa uwepo hapo.
Afadhali ujue wazi kabisa kuwa kazi unayofanya umeizidi sifa kuliko iwe ya kawaida lakini uwezo wako ushindwe kuonekana.Kazi inapofikia hatua hiyo maana yake nafasi ya wewe kukua kiujuzi itakuwa ndogo.
RAHA YA MAISHA NI KUFURAHIA KITU UNACHOFANYA, IWE INAKUINGIZIA KIDOGO AU KIKUBWA FURAHA NDIO HUWA KIPAUMBELE.
KUFANIKIWA NI ZAIDI YA KUWA KIPATO KIKUBWA NA MALI.
ANZA LEO KUTAMBUA KAZI UNAYOIPENDA NA UANZE KUISHI MAISHA YA MAFANIKIO KWA KUUTUMIA UWEZO WAKO KAMILI.