Spika mstaafu wa Bunge ambae pia ni Kamisaa wa Sensa Kitaifa, Anna Makinda amewataka vijana wasomi kujitengenezea uchumi wao binafsi.
Makinda amewataka vijana kutumia fursa zilizoko kwenye maeneo wanayoishi badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini au sekta binafsi.
Makinda ametoa wito huo kwa vijana wakati akizungumza Oktoba 12 na Kamati ya sensa katika kikao cha kutathimini sensa kwa Mkoa wa Arusha.
Amesema takwimu hizo ni muhimu kwa nchi kwenda kutengeneza mfumo mzima katika hatua zake za kusaidia jamii hasa kiuchumi.
“Lipo jambo kubwa nililoliona nalo ni kundi kubwa la vijana ambao hawana ajira wala hawajishughulishi na kazi yoyote ya kujiingizia kipato na ukimuuliza anasema amehitimu elimu fulani anasubiri ajira, jamani hili la kuajiriwa mtachelewa sana,” amesema Makinda
Amesema kuwa tatizo la ajira linalotupiwa serikali linaweza kutatulika na muhusika mwenyewe kwa kutazama changamoto zilizoko hata katika jamii na kuliwekea ubunifu mzuri na kuwa fursa ya ajira au kujipatia kipato kuliko kusubiri kuajiriwa.
“Mfano mzuri serikali kwa sasa inetengeneza fursa nzuri kwenye sekta ya kilimo na uzuri nchi yetu ina maeneo mengi wazi, lakini utakuta kijana msomi anasema anasubiri kuajiriwa badala atumie fursa kutengeneza ajira, nawaambia hao sio wasomi wazuri ambao Taifa linaweza kuwategemea,” amesema.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema kuwa jumla ya kaya 2,724 zilihesabiwa katika vitongoji 1,506 na kazi ilifanikiwa kwa asilimia 99.99.
Mongela amesema “kwenye kazi hii serikali ilitupatia kiasi cha Sh5.9 bilioni na tumefanikisha kazi hiyo na vifaa vyote tulivyokabidhiwa tumerudisha kasoro vishwambi vitano ambavyo vilipotea, lakini jeshi la polisi linaendelea na kazi ya kuvipeleleza vipatikane”.
Soma: Wahitimu vyuo vikuu wanavyoomba kazi za elimu ya sekondari