Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Maua ni fursa ya biashara

Maua ni fursa ya biashara

0 comments 916 views

Watu wengi wanapenda kupendezesha nyumba zao ama ofisi kwa mapambo mbalimbali ikiwemo maua.

Ama kwa hakika, bustani za maua mbalimbali zinazotunzwa vizuri ni kivutio kikubwa husasani majumbani na sehemu zingine mbalimbali.

Vijana wengi wameanzisha biashara ya kuuza maua na wengine wakifanya kazi ya kutengeneza bustani (garden) kwa utaalamu.

Biashara hii ambayo inakua kwa kasi imeweza kuwa kwamua kiuchumi kwa kuwapatia kipato.

Ukipita sehemu mbalimbali kando kando mwa barabara utaona bustani nzuri zilizopambwa kwa maua pamoja na mapambo mengine ikiwemo ukoka, makopo na vyungu vilivyotengenezwa kwa umaridadi kabisa vikingoja wateja tayari kwa kuuzwa.

Raheli Massawe ni mfanya biashara wa maua mkoani Kagera.

Anauza maua na makopo ya kupandia maua. Anasema “nilianza biashara ya kuuza maua mwaka juzi, mimi napenda sana maua, nilianza kwa kupanda nyumbani kwangu, watu wakayapenda ndipo nikaanza kuyauza.”

Raheli anasema biashara hiyo imekua ikikua siku hadi siku, watu mbalimbali wakifika nyumbani kwake wanavutiwa na maua na huwauzia.

“Nilipoanza nilikuwa nikiwauzia maua pekee, lakini sasa nauza na makopo ya kupandia maua. Huwa ninaagiza makopo kutoka Dar es Salaam na kuyauza Bukoba na ninatuma katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Biashara hii ni nzuri, haichukui muda wangu mwingi.” Anasema.

Ametoa wito kwa vijana wasio na ajira kujiajiri kwa kuwa wabunifu na kufanya biashara zitakazo wakwamua kiuchumi.

“Kwa sasa ajira ni ngumu sana, vijana wengi wamehitimu lakini hawana kazi za kufanya, vijana wengi wanashindwa kujiajiri kutokana na changamoto ya mitaji, kuna biashara ambazo haziitaji mitaji mikubwa kama hii ya maua, nawasihi vijana wajitume na kuanzisha biashara ndogo ndogo kuliko kutegemea kuajiriwa pekee.” amesema Rahel.

Akizungumzia changamoto za biashara hiyo anasema “changamoto kubwa ni aple unapoagiza maua au kusafirisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine hususani mikoani.

Unapopata mteja kutoka mkoa mwingine changamoto katika kusafirisha maua haziepukiki, wakati mwingine wasafirishaji huchelewesha mzigo na hivyo maua yanafika kwa mteja yakiwa yamenyauka. Pia wengine hawawi makini wakati wa kuyasafirisha wanachanganya na mizigo mikubwa hivyo kupelekea maua kuharibika.”

Anaeleza kuwa hali hiyo humpa hasara kwani wateja wengine hudai fidia ya ua pindi linapoharibika au kufika likiwa katika hali ambayo sio nzuri.

“Kuna baadhi ya aina za maua hayataki mitikisiko mikubwa, maua kama haya ukitaka kuyahamisha ni muhimu utoe mizizi yake ikiwa imejishika na udongo, sasa wakati mwingine unakuta wakati wa kusafirisha yanaangushwa na kutikiswa kiasi kwamba mizizi inajiachia kwenye udongo na kufanya maua hayo kushindwa kustawi vizuri,” amefafanua Raheli.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!