Spika wa Bunge Job Ndugai amesema vijana kukaa vijiweni kusubiri ajira kutoka serikalini ni mtazamo hasi.
Amewataka vijana kuacha fikra hizo potofu na badala yake watumie fursa zilizopo kuibua miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi.
“Hivi sasa kuna fursa nyingi zinazoweza kuwaingizia kipato ikiwemo ufugaji, kilimo cha zao la zabibu na bustani za mboga mboga badala ya kuendelea kukaa vijiweni kusubiri kuajiriwa.
Inasikitisha kuona vijana wanakaa majumbani na vijiweni na simu zao kwa ajili ya kuchati na kutafuta ajira na vitu ambavyo havina faida kwao wakati muda huo wangeweza kushughulika na akili kuibua miradi mbalimbali,” alisema.
Spika Ndugai alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali nchini kuhakikisha vinakuwa na bidhaa zenye ubora ili watanzania waendelee kujivunia na kuzipenda zaidi bidhaa za ndani.