Vsomo au Veta Somo ni programu ambayo inapatikana katika simu za mkononi. Programu hii imelenga kutoa mafunzo ya ufundi kwa muda mfupi zaidi (ikilinganishwa na ilivyo kawaida katika vyuo vya ufundi nchini) kwa watanzania hususani vijana wasio na ajira. Programu hii ilibuniwa miaka mitatu iliyopita na mwanateknolojia-mjasiriamali Geofrey Magila, ambaye alitajwa katika jarida la maarufu la Forbes mwaka 2017 kuwa ni miongoni mwa mabilionea wajao wenye miaka chini ya 30 barani Afrika.
Mamlaka ya elimu ya ufundi nchini (VETA) pamoja na kampuni ya simu ya Airtel ni washiriki ambao wanawezesha Vsomo kufanya kazi na kuwafikia wateja. Inaelezwa kuwa hadi sasa, zaidi ya watu 10,000 wamejisajili na programu hii huku zaidi ya watu 80 katika mikoa mbalimbali nchini wakifungua biashara zao kupitia mafunzo ya yanayopatikana katika programu hii.
Programu hii inafanyaje kazi?
Mtumiaji wa simu yenye mfumo wa Android anaweza kupakua programu hii kupitia Google Play Store kisha kujisajili bure. Baada ya hapo, anaweza kuchagua kozi ya ufundi anayotaka kujifunza. Mwanafunzi husoma kupitia programu hiyo, na kupewa mafunzo ya vitendo katika kituo cha VETA kilicho karibu yake. VETA hutoa mafunzo yao kwa kipindi cha wiki 8 lakini kupitia programu hii, mwanafunzi anaweza kusoma hadi kwa wiki mbili kisha kufanya mitihani yake. Ikiwa atafaulu basi anaweza kujiajiri kwa kutumia maarifa aliyopata na kujiingizia kipato.
Mafunzo yanayotolewa katika programu hiyo ni pamoja na misingi ya ufundi wa pikipiki, kuweka umeme, ufundi wa simu za mikononi, kuchomelea na kuunda vyuma, urembo, kutengeneza maumbo ya Alumini na Upvc, umeme wa magari, ufundi bomba, umeme wa viwandani, matengenezo ya kompyuta, huduma ya chakula na mbinu za kuhudumia wateja na kuoka na kupamba keki.
Baada ya mwanafunzi kuhitimu masomo yake, hupewa cheti sawa na mwanafunzi aliyesoma kozi ya wiki nane. Pia wahitimu wanatambulika na mamlaka zote nchini zinazohusika na masomo ya ufundi yanayofundishwa kupitia programu hiyo kwa mfano Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma na Nishati (EWURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Gharama ya kila kozi ni Sh. 120,000, kiasi ambacho kimepunguzwa kwa 60% ikilinganishwa na gharama zinazotozwa kwa wanafunzi wa kawaida wa VETA. Gharama hizo hulipiwa kupitia Airtel Money. Mlipaji anatakiwa kupiga *150*60# ili kuweza kukamilisha malipo yake.
Pamoja na hayo, VETA na Airtel wana mipango ya kuwezesha watumiaji wa mitandao mingine kutumia programu hiyo na kurahisisha suala la ada ambalo limekuwa likikwamisha wadau wengi kupata mafunzo hayo na kunufaika kiuchumi.
Muda umefika kwa vijana kuchangamkia fursa zinazokuja kupitia teknolojia mbalimbali zinazovumbuliwa nchini na nje ya nchi ili kuweza kujikimu kimaisha na kuweza kukuza uchumi wa nchi hususani wakati huu ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa viwanda. Taifa lolote hujengwa na vijana.