Home AJIRA Wahitimu vyuo vikuu wanavyoomba kazi za elimu ya sekondari

Wahitimu vyuo vikuu wanavyoomba kazi za elimu ya sekondari

0 comment 196 views

Ndoto za vijana wengi huwa ni kuajiriwa katika kampuni ama taasisi mbalimbali pindi tu wamalizapo masomo yao husasani elimu ya juu.

Ugumu wa soko la ajira kwa sasa imekuwa ni moja ya sababu kubwa inayozima ndoto ya baadhi ya wahitimu ambao idadi yao kubwa ni vijana pamoja na ujuzi na elimu waliyoipata kwa kipindi kirefu.

Changamoto hii inapelekea wahitimu wengi kuomba nafasi za kazi hata zile ambazo hawakusomea ama kuwa na ujuzi nazo ili mradi tuu waweze kupata ajira huku wakiwa na matumaini ya kupata kazi bora zaidi inayohusiana na taaluma zao.

Ugumu wa soko la ajira umepelekea wahitimu wengi kutumia vyeti vya elimu ya sekondari kidato cha sita au cha nne endapo tuu ataona ama kusikia tangazo la ajira kwa watu wenye kiwango cha elimu hiyo.

Ipo wapi sasa sababu ya kusoma kwa kiwango cha elimu ya juu kama hawawezi kupata sehemu mahususi ya kutumia elimu ambayo wengi wao wamehangaikia kwa muda mrefu.

Baadhi ya wahitimu wanasema hali ngumu ya maisha pamoja na ukosefu wa ajira huwafanya kuweka kando elimu na vyeti vyao na kufanya kazi yoyote ili mradi mkono uende kinywani, yaani wapate walau mlo maisha yaendelee.

Mhitimu kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam Juma Said (sio jina lake halisi) anasema “nilianza kutafuta kazi miezi michache kabla sijamaliza masomo yangu lakini mpaka sasa bado sijafanikiwa.

Niliona tangazo la kazi za wakala wa uchaguzi ukizingatia huu ni mwaka wa uchaguzi nikaomba nafasi hizo, ilinilazimu niweke kando degree yangu na kutumia vyeti vyangu vya elimu ya sekondari.”

Anaeleza kuwa sio tuu kutoandika kiwango cha elimu zao, pia wanapunguza elimu kulingana na soko la ajira.

Mhitimu mwingine anasema yupo tayari kuandika ana elimu ya kidato cha sita au cha nne ili tuu apate ajira.

Mwingine anasema alipata hofu juu ya soko la ajira pale alipokosa hata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

“Nilihangaika sana kupata ofisi ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field) kwani ofisi nyingi ukipeleka maombi wengine wanasema hakuna na fasi na wengine husema hawapokei vijana wa mafunzo kwa vitendo, kwa kweli hali ya ajira kwa sasa ni changamoto sana naona bora nirudi kijijini,” anasema.

Benki ya Dunia (WB) inakadiria vijana wapatao 800,000 huingia katika soko la ajira Tanzania kila mwaka lakini ni takriban asilimia 10 tu ndiyo hufanikiwa kupata kazi.

Hii inaonesha ni jinsi gani idadi kubwa ya vijana hubaki mitaani bila ajira na wachache kati ya hao huweza kujiajiri wenyewe.

Imewachukua miaka kadhaa wahitimu wengi kupata ajira rasmi. Licha ya kuwepo kwa kampuni, taasisi ama watu binafsi wanaotafutia watu ajira, bado ni changamoto kwani baadhi yao huhitaji malipo ya fedha kwa ajili ya kuwatafutia kazi.

Vijana hawa watapata wapi fedha za kulipia kutafutiwa kazi ili hali wao hawana kazi na wanatafuta kazi za kuwaingizia kipato?

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter