Na Mwandishi wetu
Benki ya KCB Tanzania imefanya uzinduzi mpya katika tawi lake la Stone Town Zanzibar ambayo kuanzia sasa itajulikana kama KCB Sahl Bank. Benki hiyo itatoa huduma zake kwa kufuata nyayo za kiislamu hivyo wateja hawatatozwa riba.
Akiwa katika hafla ya uzinduzi huo, Cosmas Kimario ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB amesema benki hiyo itakuwa ya kwanza nchini kutoa huduma za kibenki zinazofuata Sharia ya Kiislamu katika akaunti za kuweka amana na mikopo mbalimbali ya kibiashara pamoja na watu binafsi, wanafunzi na watoto.
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohammed ametoa pongezi za dhati kwa benki hiyo na kuishukuru kwa kujitolea ili kuboresha sekta mbalimbali kama vile elimu, afya, mazingira na watoto yatima ambazo zina umuhimu mkubwa katika jamii.