Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendeleza jitihada ya kukuza matumizi ya fedha kidigitali badala ya pesa taslimu ili kuendana na madadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea hivi sasa.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo Machi 06, 2025 jijini Dr es Salaam wakati akifungua rasmi Mhadhara wa Kumbukumbu ya Gilman Rutihinda, Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) aliyefariki mwaka 1993.
“Ni lengo la Serikali kuhakikisha kwamba watu wengi zaidi wanatumia njia za kidigitali katika huduma za kifedha, zikiwemo kufanya biashara, kufanya malipo, manunuzi pamoja na kuagiza bidhaa,” amesema.
Waziri Dkt. Nchemba amemsifu Gavana Rutihinda kwa kuweka msingi wa uchumi wa kisasa wa Tanzania kupitia mageuzi katika sekta ya fedha kuwa huru na inayoendeshwa kwa nguvu za soko.
“Mageuzi yake yaliibua ubunifu, ujumuishi na uendelevu kwa kukuza ushindani, kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha na kuhakikisha uthabiti endelevu, amesema.
Aidha, alisema Serikali inazungumza na wadau wengine wanaofanya shughuli za kidigitali kupunguza gharama za huduma zao ili kuvutia watu wengi zaidi kutumia mifumo ya kidijitali badala ya pesa taslimu ili kuongeza ufanisi, kuokoa muda na hatari ambazo zinaweza kutokea kwa watu kubeba na kutumia pesa taslimu.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba alisema kumbukumbu ya marehemu Gavana Rutihinda inawapa nafasi ya kutafakari masuala muhimu yanayoikumba sekta ya fedha katika wakati huu.

Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba.
“Inakadiriwa kwamba asilimia 90 ya miamala katika uchumi inategemea pesa taslimu. Mabadiliko kutoka matumizi ya pesa taslimu hadi kidigitali katika uchumi ni suala la lazima. Mabadiliko hata yana nafasi ya kuchangia kuongeza ustahimilivu, uthabiti na ujumuishi katika sekta ya fedha” ameeleza Gavana Tutuba.
Amesema kupunguza matumizi ya pesa taslimu kutaongeza ufanisi, uwazi na kupanua wigo wa watu wanaofikiwa na huduma za kifedha, hasa jamii ambazo zimeachwa nyuma katika kupata huduma rasmi za kifedha.
Kauli mbiu ya mhadhara wa tisa wa Kumbukumbu ya Gilman Rutihinda ni Kuhamasisha mabadiliko kuelekea uchumi wa kidigiti: Fursa za ubunifu na huduma jumuishi za fedha.