Shirika la ndege Tanzania (ATCL) linatarajia kuanza safari zake za nje kuanzia kesho ikiwa ni katika kutekeleza azma yake ya kulitambulisha shirika hilo kimataifa, sambamba na kutangaza fursa za kiuchumi, uwekezaji, na utaliii zinazopatikana nchini.
kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi, shirika hilo linatarajia kuanza safari zake wiki ijayo katika nchi saba ikiwemo Afrika Kusini, huku safari za Bujumbura na Entebbe zikitarajiwa kuanza kesho hadi Agosti 30.
Soma Pia ATCL kutua Entebbe,Bujumbura
Akielezea ratiba ya safari hizo Matindi amesema kuwa safari za kwenda Entebbe zitakuwa Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili na zitaanzai Dar es salaam, Kilimanjaro na Arusha, huku safari za Bujumbura zikifanyika siku za Jumanne, Alhamisi na Jumapili kutokea Dar es salaam na kupitia Kigoma, pamoja na zile za nje ya bara la Afrika ambazo ni Mumbai (India), Bangkok (Thailand), Guangzhou (China) kupitia Dar es salaam ambazo ratiba zake hazijatajwa rasmi.
Soma Pia ATCL kuimarika kufikia 2023
“Tutaendelea kupanua wigo wa huduma za nje ya Afrika ili kuibua fursa za uwekezaji, biashara na utalii zinazotokana na kuanza kwa huduma za safari hizi za ndege katika nchi hizi za Afrika Mashariki”. Ameeleza Matindi.
Jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na serikali katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais John Magufuli kuboresha huduma za ATCL kupitia ununuzi wa ndege za shirika hilo ambapo mpaka sasa ndege nne mpya zimeshanunuliwa na serikali na kuletwa nchini, ikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner ambayo ni ndege kubwa zaidi kununuliwa katika historia ya Tanzania ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 262.