Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Josephat Kagirwa amesema shirika hilo litaanza kufanya safari za kwenda Entebbe nchini Uganda na Bujumbura, Burundi mwishoni mwa mwezi huu ikiwa ni jitihada za shirika hilo kupanua wigo wa biashara baada ya kufanya vizuri katika soko la ndani na vilevile kukuza utalii.
Ndege zitakazofanya safari hizo ni pamoja na Bombardier Dash 8 Q400 zilizo na uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja. Safari za kwenda Entebbe zinatarajia kuanza Agosti 26 huku zile za Bujumbura zikianza Agosti 30, mwaka huu.
“Ndege zote mbili zitakuwa zikianza safari zake kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi, lakini ndege inayoenda Entebbe itakuwa ikirejea Dar es Salaam saa 8:50 mchana na ile inayoenda Bujumbura itakuwa ikirejea Dar es Salaam saa 10 jioni”. Amefafanua Kagirwa.
Aidha, Kagirwa ameeleza kuwa kila ndege itakuwa na daraja la biashara na daraja la kawaida ambapo kwenye daraja la biashara litakuwa na viti sita na viti vingine 70 ni kwa ajili ya daraja la kawaida akisisitiza kuwa ATCL imeweka bei nafuu kwa wasafiri wa Entebbe na Bujumbura na kwamba, utaratibu wa kupata tiketi ni ule ule.