Wakati sera kuu ya Tanzania ni vijana na wanawake kujiajiri, upatikanaji mgumu wa mtaji unazuia maendeleo. Serikali imefanya mengi ili kuongeza upatikanaji wa mtaji kwa makundi maalum kama wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hata hivyo mengi zaidi yanahitajika kufanywa.
Hadi sasa, serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imerahisisha mahitaji ya ukopaji kwenye mabenki na kwa kufanya hivyo, serikali imerahisisha upatikanaji wa mikopo kwa masharti nafuu.
Lakini, ingawa biashara nyingi zinafaidika na urahisishwaji wa masharti ya mikopo, wanawake na vijana ambao hawana biashara au wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi, upatikanaji wa mikopo ya benki bado ni changamoto kubwa.
Ili kukabiliana na kikwazo hiki, serikali imeanzisha mchakato wa kusaidia vikundi vya vijana na wanawake kupata mtaji. Vijana na wanawake wanapaswa kuunda vikundi na kutengeneza mpango wa biashara ilikupata mikopo isio na riba kupitia mamlaka ya serikali za mitaa.
Kwa kuchagua biashara zinazohitaji mtaji mdogo, vijana na wanawake sasa wanaweza kufaidika na mchakato huu. Kwa mfano, biashara za uuzaji wa moja kwa moja hazihitaji mtaji mkubwa kuanzisha na pia zinakupa uhuru wa kufanya biashara zingine kwa wakati mmoja.
“Kuuza moja kwa moja ni njia ya mauzo inayotumiwa na makampuni kutangaza bidhaa zao moja kwa moja kwa watumiaji wa mwisho kupitia mjasiriamali mwenyewe,” alifafanua Biram Fall, Meneja Mkuu wa Kanda wa QNET katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Katika mawasiliano ya vyombo vya habari mapema wiki hii, Bwana Fall alieleza kuwa mustakabali wa uchumi wa Afrika unategemea biashara ndogo ndogo na kujiajiri kwa vijana na wanawake hususan kupitia biashara za moja kwa moja na mtandaoni.
“Biashara za kidijitali zinazidi kukuwa kwa kasi sana na zina nafasi kubwa katika uchumi wa sasa. Biashara za uuzaji wa moja kwa moja zinawapa vijana na wanawake fursa za kujiajiri kwa mtaji mdogo tu,” alisema.
Biashara za mauzo ya moja kwa moja, ni biashara ambapo mjasiriamali anauza bidhaa moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji kwenda kwa mtumiaji wa mwisho. Biashara za mfumo huu zinafanyika mtandaoni ambapo muuzaji anaweza kutafuta wateja na kuuza bidhaa bila kukodi eneo la kufanyia biashara hivyo kupunguza gharama za uanzishaji wa biashara yenyewe.
Pia, biashara za moja kwa moja zinaweza kufanyika kupitia maonyesho madogo madogo maofisini au majumbani ambapo mjasiriamali anapeleka bidhaa sehemu husika na kuwauzia wahusika.
Bidhaa chini ya mfumo huu huwa ni bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na zilizodhibitishwa na mashirika ya ubora duniani na nchini.
Kwa urahisi wa mfumo huu, biashara za moja kwa moja ni chanzo cha kuongeza kipato mbadala kwa wanawake na vijana walioajiriwa au ambao tayari wana biashara zingine.