Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amepokea Mpango kazi wa shirikisho la Bodaboda wa mkoa huo unaolenga kusajili idadi ya waendesha bodaboda, vituo pamoja na kuwaingiza kwenye mfumo rasmi.
Hatua hiyo imekuja Baada ya Shirikisho la bodaboda kubaini kuwa serikali imekuwa ikikosa mapato ya takribani Sh. bilioni 7 kila mwaka kwa kukosekana kwa mpangilio mzuri wa uendeshaji wa shughuli hiyo.
Shirikisho limebainisha kuwa mapato ya vituo yamekuwa yakiingia mifukoni mwa wajanja na sio serikalini.
Kutokana uholela huo shirikisho limeoma ni wakati muafaka kwa serikali kuanza kupata mapato yatokanayo na kazi ya Bodaboda kwa kuwa ni ajira rasmi.
Akipokea Mpango kazi huo, RC Makalla amesema mbali na kuwa mpango huo utaweka mazingira bora ya biashara pia utasaidia serikali kukusanya mapato na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.
Aidha, RC Makalla amelielekeza shirikisho kumpatia ratiba ya siku watakazokwenda kuwasilisha Mpango kazi ngazi ya Wilaya ambapo amewaelekeza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuratibu jambo hilo kwa kuhakikisha linatekelezwa mpaka ngazi ya Mtaa.
Hata hivyo RC Makalla amepongeza hatua ya Shirikisho kupata mdau atakaetoa magari kwaajili ya kutoa huduma kwa waendesha bodaboda pindi watakapopatwa na majanga ya ajali na misiba.
Mwenyekiti wa shirikisho la Bodaboda Mkoa wa Dar es salaam Said Chenja ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara ya bodaboda.