Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, ametoa wiki mbili (siku 14) kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kurekebisha mifumo yao ya kielektroniki ya kutoa huduma. Waziri Kakunda amefikia uamuzi huo baada ya kutembelea wakala huo na kueleza kuwa, mifumo yao ya kielektroniki imekuwa ikilalamikiwa na wananchi wengi hasa katika siku za karibuni.
“Ndani ya wiki mbili nimekuja tena hapa kwa sababu kuna sababu maalum, udhaifu mkubwa uko kwenye mifumo kuliko uhalisia. Kila nikipokea simu 10 za wafanyabiashara nane zinalalamikia BRELA hili ni tatizo”. Amesema Waziri huyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Emmanuel Kakwezi, amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu wa watumishi 51 pamoja na mfumo kutokuwa imara.
“Kuna changamoto ya mtandao wa ORS katikati ya kazi unaweza kuzimika. Mteja anatuma maombi lakini haionekani na sisi tunaweza kumjibu lakini haoni”. Amefafanua Kakwezi.