Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI), wadau na wafanyabiashara kwa pamoja wameijadili bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 iliyotangazwa bungeni hivi karibuni.
Katika mjadala huo moja ya maadhimio yaliyofikiwa ni pamoja na kuiomba serikali kurekebisha ukusanyaji wa baadhi ya kodi zilizobainishwa katika bajeti hiyo. Kuongezeka kwa ushuru wa forodha katika uingizaji sukari na mafuta ghafi imekuwa ni kilio kwa wadau hao huku wakisisitiza inaweza kushusha uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.
Dk Samwel Nyantahe ambaye ni Mwenyekiti wa CTI amesisitiza kuwa, japo lengo la kuongeza ushuru huo ni kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza uzalishaji hasa wa ndani, bado kunaweza kusilete matokeo tarajiwa hivyo kuwaathiri wawekezaji wanaotegemea malighafi hizo.
Kikao hicho pia kimeipongeza serikali kwa kujibu zaidi ya asilimia 70 ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa hivyo wanategemea jambo hilo litawahamasisha wawekezaji.
Bajeti kuu ya serikali ilisomwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango ambapo licha ya kuzungumzia mambo mbalimbali pia iliongeza ushuru wa forodha wa mafuta ghafi ya kula kutoka asilimia 25 hadi 35 na huku ushuru wa sukari nao ukipandishwa kwa asilimia 15. Pamoja na hayo, Waziri Mpango pia alibainisha kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo za kike, malighafi za vyakula vya mifugo na vifungashio vya dawa.