Home BIASHARA Epuka changamoto hizi, fanya haya

Epuka changamoto hizi, fanya haya

0 comment 113 views

Ili kuweza kufikia malengo katika kila jambo, lazima kutakuwepo na changamoto mbalimbali. Katika upande wa biashara, ni wazi kuwa wafanyabiashara hupitia changamoto za aina yake na mara nyingi changamoto hizo zinampa mtu nguvu na ujasiri zaidi ili kuweza kusonga mbele. Kiukweli, changamoto zipo nyingi na kutokana na hilo, watu wengi wamepata nguvu ya kuweza kufanya kazi kwa juhudi zaidi na kufanikiwa.

Hizi ni baadhi ya changamoto na jinsi ya kukabiliana nazo.

Mtaji

Hakuna mfanyabiashara ambaye anaweza kukiri kuwa mtaji alionao kwa ajili ya biashara yake unamtosha. Hii hutokana na mahitaji kuendelea kujitokeza hata baada ya kuanzisha rasmi biashara. Nini kifanyike ikiwa moja ya changamoto katika biashara ni mtaji? Kwanza kabisa, mjasiriamali anatakiwa kufahamu kuwa sio lazima kuwa na mtaji mkubwa ili kuendesha biashara. Jambo la msingi zaidi ni kuwa na mikakati mizuri itakayosaidia biashara kukua na kufanikiwa.

Kuna maeneo mbalimbali ambayo mtu anaweza kupata mtaji kwa ajili ya kuanzisha au kupanua biashara yake, maeneo hayo yanaweza kuwa katika taasisi za kifedha kama benki, vikundi vya fedha nk. Aidha, unaweza kupata mtaji kwa ndugu jamaa na marafiki. Vilevile mfanyabiashara anaweza kuuza vitu vyake vya thamani ambavyo havina umuhimu sana kwa kipindi hicho na kuelekeza fedha katika biashara yake. Pamoja na hayo, mfanyabiashara anaweza  kujiunga na vikundi ili kuweza kupata mtaji au kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa jinsi ya kutatua changamoto hii.

Ushindani

Biashara yoyote isiyo na ushindani inatakiwa kujitathmini mara mbili. Bila ushindani ni vigumu kukua, kujifunza na kujitofautisha sokoni. Ushindani sio suala la kuogopa na badala yake, mfanyabiashara anashauriwa kuwa mbunifu ili kuwavutia wateja zaidi. Pia ni muhimu kujitangaza katika majukwaa mbalimbali kwa mfano mitandao ya kijamii, televisheni, redio, magazeti ili kuweza kuwajulisha wateja kuhusu bidhaa au huduma zako. Baada ya kujitangaza, bei inaweza kupelekea kupata wateja wengi. Unapouza kwa bei rafiki ni dhahiri kuwa watu wengi watanunua bidhaa zako hivyo kabla ya kupanga bei fanya utafiti kuhusu kundi la wateja ambao unataka kuwalenga na pangilia bei kutokana na uwezo wao kifedha.

Masoko

Bila masoko hakuna faida katika biashara. Ndio maana inashauriwa kuwekeza katika masoko ili kuweza kupata wateja kutoka sehemu mbalimbali. Ni muhimu kuajiri mtu mwenye ujuzi wa masoko ili kupata ushauri kuhusu mauzo ya bidhaa zako na kuweza kuzitangaza sokoni. Mbali na kufanya hivyo, ni muhimu kujua wateja wako kabla hujakamilisha kila kitu kuhusu bidhaa yako. Hii italeta urahisi wa kujua ni kundi lipi litahamasika kununua zaidi.

Elimu

Tambua kuwa elimu haina mwisho. Wakati mwingine watu wanakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu biashara wanayofanya lakini kuwa na nafasi ya kujifunza kila wakati ni siri kubwa ya mafanikio yao. Endelea kujifunza kila siku kwa sababu mambo hubadilika kila siku. Tumia muda mchache kila siku au hata kila wiki kujifunza mambo mapya kupitia mitandao ya kijamii, semina na maonyesho mbalimbali ili kuweza kupata kitu kipya ambacho kitafanya uweze kupata urahisi wa kuendeleza biashara yako.

Mgawanyo wa kazi

Mfanyabiashara mwenye malengo ya kukua na kufanikiwa anatakiwa kujua kuwa hawezi kufanya kila kitu mwenyewe. Kadri biashara inavyokuwa ndivyo umuhimu wa mgawanyo wa kazi unavyoongezeka Unaweza kuwa na uelewa wa kila mchakato katika biashara lakini kuajiri watu wenye ujuzi na utaalam fulani kutarahisha ufanisi wa kazi na kuleta mafanikio zaidi. Kwa mfano unaweza kuwa na ujuzi wa kuzalisha biashara lakini huna ujuzi wa kufanya masuala ya mahesabu. Hapa unaweza kutafuta mtaalamu wa suala hilo ili kuhakikisha mtiririko wa fedha unakwenda sawa.

Changamoto ni nyingi katika biashara na huwa zinakuja katika mtindo tofauti. Jambo la msingi ambalo kila mjasiriamali anatakiwa kufanya ni kuchukulia changamoto hiyo kama ni  jambo la mpito, kuepuka kujilaumu au kuwalaumu watu wengine na kuchukua hatua ili kuweza kusuluhisha changamoto hiyo na kusonga mbele.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter