Kuanzisha biashara yako mwenyewe ni kitu kizuri kwani unatekeleza wazo au mawazo uliyonayo kwa vitendo na kuwa mmiliki wa mradi wako mwenyewe. Licha ya mazuri mengi, hiki ni kipindi ambacho unaweza kupitia changamoto mbalimbali. Kuna vitu vitaenda kama ulivyopanga na kuna vingine vitakwama. Unapoanzisha biashara ya aina yoyote ile, epuka kufanya makosa haya matatu:
Kufungua ofisi moja kwa moja: Kama ndio kwanza unaanza biashara yako, hakuna haja ya kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kukodi au kujenga ofisi. watu wengi wanafikiri kuwa unapokuwa na ofisi unakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kupata mafanikio lakini hii haitakiwi kufanyika katika hatua za mwanzo kabisa hususani ikiwa bajeti yako hairuhusu. Biashara nyingi tu siku hizi zinafanya kazi kutoka nyumbani, ni kitu cha kawaida na unaokoa gharama. Hauhitaji ofisi rasmi pindi unapoanzisha tu biashara yako.
Kujitangaza kwa kila mtu: Ukweli ni kwamba sio kila mtu ni mteja wako. Katika kila biashara au wazo la biashara, lazima kuna walengwa wakuu wa bidhaa au huduma husika hivyo badala ya kutumia nguvu na hata fedha nyingi kujitangaza kwa kila mtu, wekeza katika kujitangaza kwa watu sahihi. Biashara mpya inapojitangaza kwa kila mtu, inaweza kukosa wateja wa uhakika na huo ni mwanzo mgumu ambao unaweza kupelekea kufunga biashara. Ni muhimu kuhakikisha unajitangaza kwa kundi la watu sahihi maana kwa kufanya hivyo, unakuwa na uhakika wa kupata wateja kila siku.
Kukosa mpango maalum: Kama mpango wako ni kuanzisha tu biashara bila kuwa na mikakati ambayo itakuongoza na kukuwezesha kufikia malengo yako basi una wakati mgumu. Mipango ina nafasi kubwa katika maendeleo ya biashara. Ni lazima ufahamu kile unachofanya badala ya kubahatisha. Kabla hujaanzisha biashara yako, jiulize umejipanga vya kutosha? Umejiandaaje na changamoto? Ikiwa mambo yako yataenda tofauti na ulivyotarajia utachukua hatua gani? Unapokuwa na mpango maalum, unakuwa na picha halisi ambayo inakusaidia kusonga mbele hata pale mambo yanapokuwa magumu.
Kama unafikiria kuanzisha biashara, ni muhimu kufanya utafiti wa kina na kuepuka makosa kama hayo (hapo juu) ambayo yanafanywa na wengi. Sio lazima ufanye mambo yaliyo nje ya uwezo wako ili kufanikiwa. Unaweza kutumia kidogo ulichonacho na kupata matokeo makubwa. Jifunze kutokana na makosa ya wengine, kuwa na mpango maalum na fanya kazi kwa bidii. Ukizingatia yote hayo bila shaka utafanikiwa.