Home BIASHARA Faida za kuanzisha biashara ukiwa na umri mdogo

Faida za kuanzisha biashara ukiwa na umri mdogo

0 comment 133 views

Ni kawaida kusikia watu wanasema kuwa wanahitaji kuwa na uzoefu kabla ya kuanzisha kampuni au biashara. Mtazamo huo unaweza kuwa umefanya kazi kwa baadhi ya watu lakini kuna faida nyingi za kuanzisha biashara wakati bado una umri mdogo.

Hizi ni baadhi ya faida zake:

Mafunzo

Kuanzisha biashara au kampuni humpa kijana fursa ya kujifunza na kupata uzoefu. Pia kijana anapata nafasi ya kujua ulimwengu wa biashara na kujitambua yeye ni nani na ni vitu gani anaweza kufanya. Kwa kuanza biashara ukiwa mdogo lazima utafanya makosa, lakini pia una nafasi ya kujifunza kutokana na makosa hayo. Inawezekana biashara hiyo isifanikiwe lakini  hiyo haimaanishi kuwa ndio mwisho wa safari yako ya ujasiriamali kwa sababu wengi hupenda kujaribu mambo mapya kila siku. Hata katika biashara yako, inakuwa rahisi kuchangamkia fursa nyingine na kuendelea kujijenga.

Muda

Siku zote kuanza mapema jambo lolote huwa ni rahisi zaidi na mtu huanza kupata matokeo mapema. Kwa mfano wahitimu wengi wanaojiajiri huanza kupata matokeo katika biashara zao mapema kuliko wale ambao baada ya kuhitimu wanasubiria kuajiriwa kwani kwa kusubiri muda unaenda na mabadiliko yanaendelea kufanyika jambo ambalo angeweza kulifanya kwa urahisi baada tu ya kuhitimu linaweza lisiwe rahisi tena kulifanya mbeleni, pia anaweza kupata ajira na kulipwa fedha kidogo ikilinganishwa na elimu yake. Kuanza mapema mara nyingi humsaidia mtu kupata maendeleo mapema zaidi kwa namna moja au nyingine.

Majukumu

Unapokuwa mdogo hata majukumu huwa machache na mara nyingi unakuwa huna watu wengi wanaokuangalia na kukutegemea. Kadri muda unavyokwenda, majukumu huongezeka zaidi hivyo kwa kuanza biashara wakati bado ni kijana unajipa nafasi ya kufanikiwa au kushindwa kabla hujaanza kutegemewa na watu wengine.

Mtandao

Ukiwa kijana ni rahisi kuwa na muda wa kujenga mtandao na uhusiano na watu wengi. Kati ya mambo muhimu katika biashara ni mtandao kwani una majukumu machache basi inakuwa rahisi kujichanganya na watu wengine ambao tayari wameshapiga hatua. Pia kwa kutengeneza uhusiano na watu wengine ni rahisi kushirikiana na watu hao mbeleni na kufanya mambo makubwa zaidi.

Uzoefu

Mara nyingi waajiri hupendelea watu wenye uzoefu, hivyo ikiwa biashara yako imeshindikana na unataka kuajiriwa ni rahisi kupata kazi kwa sababu waajiri wanajua ni kiasi gani kinachukua kumiliki na kuendesha biashara hivyo wataona kuwa kuna umuhimu wa kukuajiri kutokana na uzoefu wako.

Aidha, ni rahisi kwa watu kuwasamehe vijana kuliko watu wazima kwa sababu wanaelewa huu ni muda muafaka wa kujifunza. Kuanza biashara ukiwa na umri mdogo inaweza kuwa jambo la kuogopesha lakini unachotakiwa kujua ni kwamba hakuna muda muafaka ikiwa unataka kutimiza malengo yako. Anza sasa!!

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter