Home BIASHARA Faida za kununua bidhaa mtandaoni

Faida za kununua bidhaa mtandaoni

0 comment 125 views

Mtandao wa intaneti unaendelea kurahisisha ufanisi wa biashara duniani. Kupitia majukwaa mbalimbali kama Amazon, Flipkart, Jumia, na mengine mengi maduka ya mtandaoni yameweza kutangaza bidhaa zao ili kuweza kufikia wateja wengi zaidi kutoka maeneo mbalimbali duniani. Ingawa watu wengi bado wanaogopa kufanya manunuzi ya bidhaa mtandaoni, kuna wengine wameshajenga utamaduni huo bila uoga. Kila kitu kina mazuri na mabaya yake, hivyo zifuatazo ni faida za kufanya manunuzi mtandaoni:

Ununuzi wa bidhaa kupitia mtandao wa intaneti ni rahisi sana. Hakuna haja ya kujiandaa na kwenda kutembelea maduka mengi kupata bidhaa unazohitaji. Kupitia majukwaa yanayojumuisha maduka mbalimbali mteja anaweza kufanya manunuzi muda wowote na mahali popote kwa kutumia simu janja au hata kompyuta. Hii husaidia mteja kuendelea na shughuli zake huku akipata bidhaa anazohitaji. Jambo la msingi ni kuwa na programu ya maduka ili kuweza kufanya manunuzi muda wowote.

Katika maduka ya kawaida huwa kunakuwa na kiasi kikubwa cha bidhaa zinazouzika kwa haraka huku katika maduka ya mtandaoni mteja anakuwa na fursa ya kuchagua bidhaa mbalimbali na kulinganisha bei kutoka katika maduka tofauti kisha kuweza kufanya maamuzi ya kununua bidhaa husika. Pia katika maduka ya kawaida mteja anaweza kuwa anataka bidhaa fulani lakini bidhaa hiyo ikawa haipo hali ambayo inaweza kupelekea mfanyabiashara aidha kumshauri mteja kununua bidhaa nyingine ambayo anaweza kuwa hana uhitaji nayo, au mteja anaweza kuahirisha manunuzi yake. Katika maduka ya mtandaoni kila bidhaa huwepo ikiwa ni pamoja na zile za msimu.

Kuna baadhi ya bidhaa ambazo wateja hupendelea kununua kwa faragha kwasababu si kila mtu anatakiwa kujua kama ununuzi huo unafanyika. Hivyo kupitia maduka ya mtandaoni mteja anaweza kununua bidhaa hizo kwa urahisi mchakato  mzima hufanyika baina ya mteja na mfanyabiashara bila uwepo wa hadhira nyingine.

Wafanyabiashara wa mtandaoni hutoa ‘warranty’ kwa wateja pindi wanapokuwa wamenunua bidhaa. Hivyo mteja anakuwa na uhakika wa kupata kile anachokitaka, na ikiwa matarajio yake hayajakamilika kupitia dhamana mteja anaweza kubadilishiwa bidhaa husika ili kuweza kupata bidhaa itakayomridhisha.

Watu wengi hawapendi msongamano,ukosefu wa sehemu za kuegesha magari na foleni madukani, hasa katika msimu wa sikukuu. Hivyo ili kuepukana na changamoto hizo, umuhimu wa maduka ya mtandaoni ndio unapokuja. Kwa kuagiza bidhaa mtandaoni unaepukana na kupoteza muda, unaepukana na misongamano huku ukipata kile unachokihitaji hadi mlangoni kwako.

Hivyo basi, kufatia zama hizi za kidijitari kuna umuhimu mkubwa kwa wateja na wafanyabiashara kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa ili kuweza kurahisisha michakato mbalimbali ya maisha na kuwekeza muda na nguvu katika masuala mengine ya muhimu ili kuendeleza uchumi binafsi na wa nchi kwa ujumla.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter