Matangazo ni muhimu wakati wa kuzindua bidhaa au huduma na hata baada ya uzinduzi ili kuelezea uwepo wa bidhaa au huduma hiyo kwa wateja (wapya na wazamani) na hata kuwavutia kununua . Imekuwa ni kawaida kuona kampuni kubwa ndio zinatumia fedha nyingi kujitangaza huku biashara ndogo zikiwa hazina desturi hiyo. Ieleweke kuwa matangazo ni muhimu kwa biashara ndogo na kubwa, na muda mwingine si lazima kujitangaza katika vyombo vya habari bali hata muonekano wa bidhaa au huduma ni tangazo tosha la biashara ambalo linaweza kuwavutia wateja au la. Hivyo ni muhimu kuwekeza katika matangazo kwa namna moja au nyingine ili kuweza kuwavutia wateja zaidi.
Mambo ya kuzingatia ikiwa unataka kutangaza bidhaa au huduma yako;
Uhalisia
Ni dhahiri kuwa bidhaa au huduma hutengenezwa kwaajili ya kusuluhisha matatizo au changamoto. Hivyo ili kuweza kuvutia wateja wengi kununua bidhaa au huduma unayotoa hakikisha kwanza bidhaa hiyo inaelezea uhalisia wa mambo ambayo yapo katika maisha ya kila siku kwa muonekano ili pindi wateja unaowalenga watakapoiona bidhaa hiyo waone bidhaa hiyo imetengenezwa kwaajili yao na kwaajili ya kusuluhisha changamoto au maisha wanazopitia. Pia hakikisha kile unachokitangaza katika vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ndio uzoefu halisi ambao wateja wataupata, hii itakusaidia kujenga msingi wa wateja ambao hawatochoka kuja kununua bidhaa zako kwasababu kupitia bidhaa hizo changamoto zao zinapata suluhisho stahiki.
Thamani
Biashara nyingi zimekuwa zikijitangaza kwa wateja wasio sahihi jambo ambalo linafanya wasione umuhimu wa matangazo. Ili kuweza kutangaza kwa wateja sahihi ni muhimu kutafakari thamani ya bidhaa au huduma unayotoa na ni wateja wa aina gani unataka kuwafikia, wana kipato gani, rika lao,jinsia na hata mawazo yao pindi watakapoona tangazo hilo. Epuka kutangaza katika hadhira ambayo haina uwezo wa kununua bidhaa yako au haina uhitaji wa bidhaa hiyo.
Mawasiliano
Unaweza kuwa na matangazo mazuri ya bidhaa au huduma yako lakini kama matangazo hayo hayaelezi jinsi ya kukupata kwamfano kwa njia ya simu, tovuti, mitandao ya kijamii nk ni dhahiri kuwa wateja wengi watapoteza hamu ya kununua bidhaa yako na kwenda kununua kwa washindani. Hivyo hakikisha katika matangazo ya biashara yako-ikiwa ni pamoja na katika vifungashio vya bidhaa kuna vielelezo vya namna ya kuweza kuwasiliana na kampuni yako ili kuweza kupata au kujua zaidi kuhusu bidhaa au huduma unayouza.
Aidha, matangazo ni muhimu katika biashara ili biashara iweze kukua na kuwafikia wateja wengi zaidi. Siku hizi biashara nyingi zinatumia mitandao ya kijamii kujitangaza kwasababu katika mitandao hiyo kuna bei tofauti tofauti ambazo hata wafanyabiashara wadogo wanaweza kumudu. Hivyo ikiwa huna bajeti ya kujitosheleza kutangaza katika vyombo vya habari vikubwa si vibaya kutumia mitandao ya kijamii kuwafikia wateja wapya.