Na Mwandishi wetu
Kamati maalum ambazo ziliundwa kuchunguza kwa kina uchimbaji na biashara ya Tanzanite pamoja na almasi zinatarajia kuwasilisha ripoti zake kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kesho mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Ofisi ya Bunge imesema baada ya taratibu za uchunguzi huo kukamilika, kamati hizo zitawasilisha ripoti zake kesho katika viwanja vya Bunge ambapo katika hafla hiyo, baadhi ya viongozi wa kitaifa watahudhuria.
Spika Ndugai aliunda kamati hizo katika mkutano wa saba wa Bunge la 11, kamati ambazo zilipewa jukumu la kuchunguza uchimbaji na biashara ya Tanzanite pamoja na almasi hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, Ndugai atawasilisha ripoti hizo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Hafla hii inatarajia kurushwa moja kwa moja kupitia chaneli ya Bunge.