Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) zimesaini mkataba wa makubaliano utakaoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Pili la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa).
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Machi 11 hadi 13, 2025.
Hafla ya utiaji saini imefanyika kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania Januari 24, 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Chana amesema Tanzania inafuraha kuwa mwenyeji wa kongamano hilo linalotarajia kukutanisha washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwamba kupitia kongamano hilo Tanzania itajifunza kutoka mataifa hayo namna wanavyofanya katika kukuza utalii wa vyakula.
“Kupitia kongamano hili tunataka kuwajengea uwezo wapishi wetu jinsi ya kutengeneza aina tofauti za vyakula ili watalii wanapokuja waweze kufurahia vyakula vya nyumbani kwao lakini pia tunahitaji kuona ni fursa gani zitakazotokana na kongamano hilo ili tuweze kujifunza utangazaji utalii wa vyakula,” ameeleza Waziri Chana.
Amefafanua kuwa Tanzania na UN Tourism zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali kwa lengo la kukuza utalii.
“Miongoni mwa maeneo tunayoomba ushirikiano kwa sasa ni katika masuala ya sera na ukuzaji ujuzi, Rasilimali Watu na Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii,” ameeleza Waziri Chana.
Katika hatua nyingine, Chana alisema Tanzania inatambua na kuthamini jukumu muhimu la Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) katika kuunda sera za kimataifa za utalii, kukuza utalii endelevu na kukuza ukuaji wa uchumi.