Katika kila biashara msingi madhubuti wa wateja ndio huleta mafanikio. Hivyo mmiliki wa biashara na hata watu wengine wanaohusika katika biashara yoyote wanatakiwa kuunda mbinu mpya kila wakati ili kuweza kuwavutia wateja wapya, kutokana na hilo biashara itakua na hata kupelekea kutimiza maono ya kampuni. Hizi hapa ni njia zinazoweza kuleta wateja wapya katika biashara:
Tengeneza mtandao
Wafanyabiashara wanashauriwa kujihusisha na mikutano au hafla mbalimbali zinazoendana na tasnia wanazojihusisha ili kuweza kukutana na watu wapya, wenye mitizamo tofauti. Kutokana na mikutano hiyo kwanza mfanyabiashara anapata fursa ya kutangaza biashara au huduma yake, pili mfanyabiashara anapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wengine na hata kupata wateja wapya. Sahara Ventures, ni moja ya kampuni ambazo zimekuwa zikiandaa hafla na mikutano mbalimbali kuhusu wajasiriamali na wafanyabiashara nchini hivyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kufuatilia matangazo mbalimbali yanayohusu tasnia zao ili kuweza kujenga mtandao madhubuti wa biashara na hata kupata wateja wapya ili kuweza kukuza biashara zao.
Shirikiana na biashara zinazoendana
Hapa mfanyabiashara anaweza kupata wateja wapya kwa kujihusisha au kushirikiana na biashara zenye misingi sawa katika upande wa wateja. Kwamfano mfanyabiashara wa nguo za akina mama na mfanyabiashara wa nguo za watoto wanaweza kushirikiana kwa kutangaza punguzo la bei kwa wateja ambao watanunua nguo kutoka katika duka moja kwenda katika duka jingine(referral).
Tumia mirejesho chanya
Kila mteja hupenda kupata huduma au bidhaa ambayo itakidhi mahitaji yake au kutoa suluhisho katika changamoto zake. Na wateja wengi hupata hamasa ya kununua bidhaa au huduma baada ya kuona watu wengine wamelidhika nayo. Hivyo mfanyabiashara makini anapaswa kuhakikisha wateja wanaridhika na kueleza uzoefu wao na huduma au bidhaa husika kwamfano katika mitandao ya kijamii au hata kwa ndugu,jamaa na marafiki ili kuweza kuvutia watu wapya kununua bidhaa au huduma husika.
‘Nunua moja,pata moja bure’
Ni dhahiri kuwa wateja hufurahia kununua bidhaa au huduma kwa bei ndogo. Hivyo tengeneza utamaduni ambao utawavutia wateja wapya kwa kupunguza bei. Hapa unaweza kuunda utamaduni ambao utawafanya wateja wako waweze kukutofautisha na washindani, kwamfano katika sehemu nyingi zinazouzwa vinywaji huwa kuna muda ambao vinywaji huuzwa kwa nusu bei wengi wamezoea kuita utaratibu huo ‘happy hour’ hivyo si lazima uwe na utaratibu sawa na watu wengine ila unaweza kufanya utafiti mdogo kutoka kwa wateja wako ili kuweza kujua vitu wanavyofurahia kisha kutengeneza utamaduni ambao utavutia wateja wengi zaidi katika biashara yako.
Shiriki katika masuala ya kijamii
Ili kuweza kuinua wasifu wako katika jamii inashauriwa kushiriki katika mambo mbalimbali ya kijamii. Kwani ni muhimu jamii inayokuzunguka kukujua kabla ya watu wengine ambao wako mbali. Sio lazima kutoa fedha, kuna mambo mbalimbali ambayo yanaweza kufanyika jamii bila uhitaji wa fedha kwamfano usafi, kutoa elimu na mengineyo. Kwa kujihusisha na jamii kila baada ya muda mfanyabiashara anapata fursa ya kuitambulisha biashara yake kwa wateja wapya na hata kuwakumbusha wateja wazamani kuwa kuna huduma au bidhaa husika.
Mbali na hayo, ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kuwasikiliza wateja kwani kwa kufanya hivyo inakuwa rahisi kujua mambo ambayo yanafanyika kwa usahihi katika biashara na mambo ambayo yanatakiwa kuboreshwa ili kuweza kukidhi mahitaji ya wateja wa zamani na wapya.