Home BIASHARA Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kukusanya maoni ya wafanyabiashara

Kamati ya Waziri Mkuu yaanza kukusanya maoni ya wafanyabiashara

0 comment 122 views

Kamati maalum ya kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini iliyoundwa na Waziri Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imeanza kukusanya maoni ya wafanyabishara kutoka sekta mbali mbali jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo inaundwa na wajumbe 14 ambapo wajumbe saba ni wawakilishi wa wafanyabiashara nchini na wajumbe wengine ni kutoka Wizara na Taasisi mbali mbali zinazohusika na biashara nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. John Jingu amesema kamati hiyo imepewa siku 14 kukamilisha kazi ya kukusanya maoni ya wafanyabishara kote nchini na kisha kuwasilisha taarifa hiyo Serikalini kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

Dkt. Jingu amepongeza mahudhurio ya wafanyabiashara na namna wanavyotoa maoni yao kwa uwazi na uhuru kwa ajili ya kuwezesha pande zote mbili kufikia muafaka wa kutatua changamoto za wafanyabiashara.

Kamati hiyo imeundwa baada ya wafanyabiashara kugoma na kufunga maduka yao ikiwa ni njia mojawapo ya kufikisha maoni yao.

‘’Natoa shukrani zangu za dhati kwa wafanyabiashara wa Dar es Salaam kwa kutuunga mkono na kutupa ushirikiano wa hali ya juu, hivyo natoa wito kwa wafanyabiashara watakaopitiwa na kamati hiyo kote nchini kutoa ushirikiano kwa kamati ili kuwezesha kupatikana kwa majawabu sahihi na kuleta mapendekezo yanayotakiwa,” amesema Jingu.

Kwa upande wake katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dr. Hashil Abdalah amesema kuwa serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni serikali sikivu hivyo ipo tayari kuwapatia wafanyabiashara nafasi ya kujadili kwa pamoja kero zao.

‘’Niwahaidi Watanzania, Rais yupo tayari kuwasaidia wafanyabiashara wote kwani ameonesha nia kubwa na kuguswa zaidi na matatizo yaliyojitokeza na kusababisha mgomo na ndio maana ameituma kamati hii ili kusikiliza kero na kisha kuziwasilisha serikalini kwa maslahi mapana ya nchi na kudumisha uhusiano uliopo baina ya serikali na wafanyabiashara,’’ ameseieitiza Dr. Hashil.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa kikao hicho ni kwa ajili ya kupata mapendekezo ya nini kifanyike na kuwashauri wafanyabiashara kutoa maoni na kero zao zote zinazowakabili ili serikali iangalie namna bora ya kuweza kuwasaidia.

Kamati hiyo imepanga kufanya mikutano kwa siku mbili kuanzia tarehe 22 na 23 Mei, 2023 Jijini Dar Es Salaam na kisha itahamia katika kanda mbali mbali za Tanzania Bara na Zanzibar na kuhitimisha kwa kufanya majumuhisho kabla ya kuwasilisha ripoti hiyo kwa Waziri.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter