Mikataba ni muhimu na hutumika kila mahali kuhakikisha mabadilishano baina ya pande mbili yanakwenda sawa. Hivyo hata katika biashara mikataba ni muhimu ili kulinda siri za biashara, sifa ya biashara, mali zilizopo katika biashara, vifaa vyako n.k.
Kwa Tanzania, serikali imekuwa ikiendelea kusisitiza kuhusu mikataba kutokana na changamoto ambazo watu wengi wamekuwa wakiendelea kuzipata kutokana na kukubaliana kwa mdomo. Licha ya jitihada hizo watu wengi hupuuzia mikataba bila kujua kuwa kuna siku watahitaji kutoa vielelezo kuhusu changamoto yoyote inayoweza kutokea kati ya mfanyabiashara na mtu wa upande wa pili. Hivyo ni muhimu kuzingatia mikataba katika kila jambo kwa sababu kutokuwa na ushahidi wa maandishi basi jambo husika litaonekana kuwa halijawahi kutokea na mtu anaweza kuleta changamoto katika biashara au mmiliki wa biashara anaweza kufanya mambo yasiyofaa, au kwa mazoea.
Ikiwa unataka kusaini mkataba na mtu kuhusu biashara hakikisha mkataba huo una vitu vifuatavyo:
- Ofa, katika kila mkataba huwa kunakuwa na ofa inaweza kuwa ofa ya kununua bidhaa au huduma, kutoa huduma au kuuza bidhaa fulani, kumuajiri mtu, kumlinda mtu na nyingine nyingi.
- Ili mkataba ukamilike lazima kuwe na sehemu ya makubaliano kati ya pande zote.
- Pia lazima kuwe na kipengele za mafikirio, kwa lugha nyingine masharti ya ofa husika. Je mnunuzi anatakiwa kulipia muda huo huo au baada ya kipindi fulani, muuzaji anapokea fedha taslimu au katika njia mbalimbali kama kwa njia ya simu, je mtu anayekuletea mzigo anatakiwa kuleta mzigo wa bidhaa baada ya muda gani? Na maswali mengine mengi kulingana na aina ya mkataba wako.
- Katika kila mkataba lazima kuwe na kipengele cha wajibu, kwa mfano labda mnunuzi anakubaliana kulipa malipo kwa bidhaa au huduma au muuzaji anakubali kutoa bidhaa au huduma vilevile wafanyakazi wanakubali kufanya kazi masaa mengi kwa wiki au kuweka siri za biashara.
- Ili pande zote ziweze kutimiza majukumu yao lazima kuwe na kipengele cha uwezo na vigezo. Ikiwa ni pamoja na kueleza kama pande zote zina umri unaokubalika kisheria kuingia katika mkataba, je watu wanaoingia katika mkataba wana akili timamu? Je, wana uwezo wa kifedha na kukubali gharama zitakazokuepo?
- Jambo la muhimu kuliko yote ni kuandika kwa maandishi mkataba. Kuna msemu husema “ikiwa haikuandikwa, haikutokea” bila ushahidi watu wanaweza kufanya kazi kwa mazoea na kufanya kazi kwa mazoea au isivyotakiwa lazima kutaathiri mwenendo wa biashara yako. Hivyo hakikisha kila mtu unayefanya naye mkataba mnaandikiana na ni vema zaidi mwanasheria akishirikishwa katika mkataba husika.
Baadhi ya mikataba ambayo imezoeleka ni pamoja na mikataba ya kazi, mikataba kuhusu ushindani (mfanyakazi na kampuni), mikataba ya usiri, mikataba ya uchuuzi, mikataba ya huduma, mikataba ya manunuzi na mingine mingi. Hivyo ikiwa unataka kusaini mkataba na mtu jitahidi kufanya tafiti zaidi katika intaneti ili kujua mambo yanayotakiwa kuwepo katika mkataba husika.
Kuwa na mkataba katika biashara kumewasaidi watu wengi katika kipindi cha madai, kumewasidia watu kufanya kazi inavyostahili na kuacha mazoea katika kazi, vil vile mkitaba imeepusha hatari mbaimbali katika biashara nyingi. Hivyo ni vema wafanyabiashara kujiwekea kawaida ya kufanya mikataba na watu wanaokabiliana nao katika biashara zao kwa njia ya maandishi ili kulinda biashara zao na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.