Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge amepiga marufuku tabia ya baadhi ya masoko kupangisha vizimba kwa madalali kisha madalali hao kuwapangishia wananchi kwa bei ya juu jambo linalowaumiza wafanyabiashara wakati lengo la serikali kujenga masoko hayo ilikuwa ni kuwasaidia wafanyabiashara na sio kuwakandamiza.
RC Kunenge ametoa onyo hilo wakati wa ziara Jijini humo ambapo pia amewaelekeza Wakurugenzi wa Manispaa zote za jiji hilo kukaa pamoja na kufanya mapitio ya bei elekezi za kupanga kwenye masoko ili kusiwe na kupishana kwa gharama za bei ya upangaji.
Aidha RC Kunenge amesema masoko yanayojengwa yakikamilika na wafanyabiashara wakapangiwa sehemu za kuuza bidhaa zao ni marufuku kwa mfanyabiashara kufanya biashara nje ya masoko au sehemu zisizo rasmi.
Akiwa kwenye Mradi wa Soko la Tandale amemtaka mkandarasi kukamilisha Mradi ifikapo mwezi wa nne mwakani kutokana na umuhimu mkubwa wa soko hilo.
Pia alimtaka Mkandarasi wa kampuni ya MECCO inayojenga soko la Kibada kwa gharama za shilingi bilioni 6.6 kuhakikisha anakamilisha soko hilo kabla ya mwezi wa tano mwakani ili wananchi waweze kunufaika na Manispaa ipate Mapato.