Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limehitimisha kampeni yake iliyolenga kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kununua bidhaa zilizodhibitishwa na shirika hilo katika wilaya za Kilwa, Nachingwea, Kilombero, Kisarawe, Korogwe, Nyamagana, Kahama, Bukoba, Tarime na Songea. Kampeni hiyo ambayo imegusa wananchi kutoka maeneo mbalimbali kama shule, stendi za mabasi, minadani na masoko ilijikita kufahamisha umma kuhusu ubora wa bidhaa pia imehimiza watanzania kuwa na mazoea ya kutoa taarifa kwa shirika hilo wanapogundua bidhaa zisizo na ubora sokoni.
Ofisa Masoko Mawandamizi wa TBS, Gladness Kaseka amesisitiza kuwa vita ya uwepo wa bidhaa zisizo na ubora unaotakiwa sokoni inagusa taifa zima kwa ujumla na sio shirika hilo peke yake.
“Kampeni hii imeweza kuwafikia wananchi 22,322 kati yao wajasiriamali 437, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 6,653 na wananchi 15,232”. Amesema Kaseka.
Pamoja na kufanya kampeni, TBS pia imetumia fursa hiyo kutoa semina wa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo nafaka, maziwa, mikate, sabuni, mvinyo, karanga, korosho, asali, mafuta ya kula pamoja na unga wa lishe kuhusu utaratibu wa kupata leseni ya kutumia alama ya ubora bure.