Home BIASHARA Mbinu 5 za kushawishi wateja

Mbinu 5 za kushawishi wateja

0 comment 117 views

Moja kati ya changamoto kubwa za biashara ndogo ni idadi ndogo ya wateja au kukosa wateja kabisa. Ni kweli kwamba unapoanzisha biashara unahitaji kuwa na uvumilivu mkubwa kwani bila shaka kuna biashara nyingine nyingi ambazo tayari zinafanya kitu hicho. Japokuwa inaweza kuchukua muda mrefu hadi biashara kuwa na wateja wa uhakika, inawezekana kabisa kushawishi wateja kuja katika biashara yako ikiwa utazingatia baadhi ya vitu muhimu.

Zifuatazo ni mbinu tano (5) ambazo mfanyabiashara anaweza kutumia ili kuhakikisha kuwa anapata wateja na biashara yake inasimama vizuri bila matatizo yoyote.

Punguzo la bei

Hii ni njia rahisi zaidi ya kuwashawishi wateja kutokana na kwamba, kila mtu anapenda kupata mahitaji yake kwa gharama nafuu. Unakuwa na punguzo la bei, unakuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana na washindani wanaokuzunguka na kupata faida kubwa katika mauzo yako. Fikiria kama biashara nyingine karibu yako zinauza bidhaa fulani kwa bei ya Sh. 10,000 na wewe ukauza bidhaa hiyo hiyo kwa bei nafuu zaidi ya Sh. 9,000. Wateja wengi zaidi watakuja kwako kutokana na tofauti ya bei na hivyo badala ya kupata wateja watano unaweza kujikuta umepata wateja kumi na tano hivyo kuuza bidhaa nyingi zaidi na kupata faida kubwa kuliko wengine.

Tatua changamoto

Biashara zenye mafanikio makubwa kote duniani zimezingatia jambo muhimu la kutatua tatizo fulani. Unapojikita katika kutatua changamoto zilizopo mahali ulipo basi bila shaka utakuwa na wateja wa uhakika kila siku na hivyo biashara yako itafanikiwa. Hii ni hatua muhimu ambayo ina mchango mkubwa katika mafanikio ya biashara. Ikiwa bidhh au huduma unayotoa haitatui matatizo yaliyopo eneo hilo kwanini watu wanunue? Kwa mfano kama unafikiria kuanzisha biashara karibu na maeneo ya shule, bila shaka biashara ambayo unatakiwa kufanya ni kuuza vifaa vya shuleni kwa ajili ya wanafunzi na walimu. Biashara nyingine yoyote tofauti na hapo itakupa wakati mgumu kwa kuwa wateja wengi wanaokuzunguka hawana uhitaji nayo.

Matangazo

Sio lazima kuwa na bajeti kubwa kujitangaza. Hata biashara ndogo zinaweza kufanya matangazo na kuwafikia watu wengi kirahisi. Unapojitangaza inakuwa rahisi kuwafikia wateja wengi zaidi na hivyo kukuza biashara yako. Baadhi ya njia (za gharama nafuu) ambazo unaweza kutumia ni pamoja na kujitangaza kupitia vifungashio, saini ya barua pepe (email signature), vipeperushi na kadi ya utambulisho wa biashara yako.

Shirikiana na biashara kubwa

Angalia uwezekano wa kufanya kazi na biashara au makampuni makubwa zaidi kama wakala au mtoaji huduma katika eneo husika. Nafasi hii hujenga uaminifu zaidi kwa wateja kutokana na huduma inayotolewa. Mfano mzuri wa kampuni unazoweza kushirikiana nazo ni kama vile Vodacom, Tigo na Airtel ambapo unaweza unaweza kuwa kama wakaa wa huduma za M-Pesa, Tigopesa na Airtel Money. Huduma hizi zina idadi kubwa ya wateja hivyo unapozihusisha na biashara yako, inamaanisha kwamba utapata wateja kwa wingi.

Mitandao ya kijamii

Leo hii, mitandao maarufu kama Facebook na Instagram imekuwa sehemu kubwa ya maisha ya watanzania walio wengi. Mitandao imekuwa sehemu ya maisha ya watanzania hivyo kama mfanyabiashara, unaweza kutumia nafasi hiyo kukuza biashara yako na kuwafikia wateja wengi kwa urahisi zaidi. Kupitia mitandao ya kijamii, una uwezo wa kupanua wigo wa huduma pamoja na bidhaa zako na kuwawezesha hata wale walio mbali kupata huduma. Ni muhimu kujitangaza mitandaoni na kuhakikisha unawahudumia wateja wako ipasavyo kwa kuwajibu kwa wakati na kuonyesha biashara.

Ukizungatia mambo haya katika biashara yako, basi utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufikia malengo, kukuza biashara na kupata maendeleo.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter