Meya wa jiji la Dar es salaam Isaya Mwita amesema mkopo wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa jengo la biashara la Machinga Complex sasa limefikia Sh. 57 bilioni. Kwa kipindi kirefu, kumekuwa na mgogoro kati ya jiji na NSSF kuhusu fedha hizo hali ambayo imepelekea kamati maalum kuundwa na kwa mujibu wa Meya Mwita, mgogoro huo upo mbioni kupatiwa suluhu.
Mgogoro kati ya jiji la Dar es salaam na NSSF uliibuka baada ya shirika hilo kutoa Sh. 12.4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Machinga Complex na deni hilo limekuwa likiongezeka mwaka hadi na mwaka mpaka kufikia Sh. 57 bilioni. Mwita amewaambia wajumbe katika baraza la madiwani kuwa hatua zinachukuliwa kutatua mgogoro huo ili kudhibiti deni hilo kuendelea kuongezeka.