Na Mwandishi wetu
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amewataarifu waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa yupo kwenye mazungumzo na Serikali ya India ili kuondoa zuio ambalo linakataza nchi yoyote kuuza zao la mbaazi pamoja na jamii zake katika nchi hiyo kwani hali hiyo inaumiza wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo hapa nchini.
Waziri Mwijage amesema kuwa mbaazi ilikuwa ikiuzwa Sh. 2000 elfu kwa kilo mwaka mmoja uliopita lakini bei hiyo imeshuka mpaka kufikia Sh. 200 kwa kilo kutokana na zuio liliowekwa na Serikali ya India. Ameongeza kuwa wauzaji wa mbaazi wa hapa nchini wamekuwa wakikosa soko, hali iliyopelekea wao kupeleka malalamiko yao katika wizara hiyo.
Hapo awali nchi ya India ilikuwa ikilima zao la mbaazi kwa uchache na walikuwa wakiagiza takribani tani milioni tano kutoka nje, lakini baada ya kuanza kulima zao hilo kwa wingi walizuia nchi nyingine kuuza nchini kwao.
Waziri huyo amedai kuwa baada ya kufanya mazungumzo na India, wameelekezwa mambo ya kufanya ili kuondoa zuio hilo siku za usoni. Ameongeza kuwa bado anaendelea kukamilisha masharti hayo ili kumaliza tatizo hilo.