Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani amemwagiza Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo kuhakikisha kuwa biashara katika soko la Kariakoo zinafanyika saa 24 pindi ujenzi wa soko hilo utapokamilika.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo wakati wa halfa fupi ya kuwaapisha viongozi wateule iliyofanyika Ikulu ndogo ya Tunguu.
Aidha, amemwagiza Waziri Jafo kufanya kazi kwa ukaribu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Mipango na Uwekezaji pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kusimamia sekta ya biashara katika soko hilo.
Amemtaka Waziri Dkt. Jafo kuhakikisha kunakuwa na mahusiano mazuri kati ya wafanyabiashara na Serikali kote nchini pamoja na kutatua kero zao hali itakayopelekea Serikali kukusanya mapato stahiki huku wafanyabiashara wakinufaika na biashara zao.
Katika kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa, Rais Dkt. Samia amemuelekeza Waziri Dkt. Jafo kufuatilia utoaji wa leseni kwa wazawa na wageni pamoja na kusajili wafanyabiashara na kuwa n aknzi data yao.
Amemtaka Kamishna wa TRA Yusuph Mwenda kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya ndani yatakayowezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi.
Rais Dkt. Samia amemtaka Kamishna Mwenda kuhakikisha mifumo ya TEHAMA kati ya TRA na Mamlaka ya Bandari inasoma ili kuweza kukusanya kodi itakayosaidia kuwekeza katika miradi ya maendeleo.
“Nakuelekeza Kamishna Mwenda kuhakikisha wafanyabiashara wote nchini wanatumia Mahine za Kielektoniki (EFD) na kuwahamasisha wananchi kudai risiti kwa manunuzi wanayofanya,” amesema Rais Dkt. Samia.