Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ametangaza nia ya kutaka kuwapa tenda Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ambalo ni Shirika la Kiserikali kwa kuwapa fedha ili Serikali ya Zanzibar iingize bidhaa sokoni.
Hii ni endapo wafanyabiashara wataendelea na uongezaji kiholela wa bei za bidhaa ikiwemo vyakula.
Rais Mwinyi ameeleza hayo wakati akihutubia waumini wa dini ya Kiislamu katika Msikiti wa Muembe Tanga Mkoa wa Mjini Unguja ambapo amesema ugumu wa kupatikana kwa mchele, unga na mafuta umesababishwa na baadhi ya wafanyabishara kuhodhi bidhaa Bandarini ili kuwe na uhaba.”
Nimewaambia wafanyabiashara sio vizuri Serikali ifanye biashara lakini mkitufikisha sehemu ambayo lazima tufanye biashara nitawataka Serikali itoe fedha tuwape ZSTC walete wao chakula wauze hapa kwasababu hatuwezi kuvumilia watu kuongeza bei kwa makusudi kwa kupenda tu kuongeza bei na nitawaambia ZSTC mwezi wa Ramadhani walete mchele kwa wingi.”
Amesema amebaini mchezo huo unaofanywa na wafanyabiashara huku akiwahakikishia wananchi kwamba hakutakuwa na uhaba wa chakula hata kwenye Mfungo wa Ramadhani.
“Sasa hivi pale Bandarini tayari kuna meli zinasubiri kushusha zaidi ya tani Elfu kumi za mchele hakuna shaka ya uhaba hata kidogo, serikali yenu itaendelea kukabiliana na changamoto hii ili tuondoe ugumu wa maisha kwa kupanda kwa bei za bidhaa katika maeneo mbalimbali,” ameeleza Rais Mwinyi.