Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwengelo kuwaelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) na wamiliki wa daladala kuhakikisha ndani ya wiki moja kuanzia leo June 28, 2021 daladala zinafika kwenye Soko la Kijichi ili kuchagiza biashara baada ya Ujenzi wa masoko hayo kukamilika na kukosa wapangaji.
RC Makalla amesema hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa Masoko Wilaya ya Temeke ambapo amesema haiwezekani Serikali itoe Bilion 4 za Ujenzi alafu masoko yageuke kuwa magofu.
“Hapa huwezi kufanya biashara kama hakuna mwingiliano wa watu, hata ungekuwa na majengo ya kila aina. Wataalamu wetu wakati mwingine mnabuni masoko mmekaa ndani mmejifungia kwenye computer, mbuni masoko ambayo yanayoendana na utamaduni wa watu wetu wa Tanzania, wewe unajenga gorofa unamwambia eti watu wa kuku mtanunua juu, apandishe na kuku akanunue juu! uliona wapi?” amesema RC Makalla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo amesema wamepokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi.
Awali, wakieleza changamoto zao, wafanyabiashara sokoni hapo wamesema ugumu mkubwa unatokana na kukosa magari katika stendi hiyo.
“Sio rahisi mnunuzi atoke huko kwa miguu aje hapa alafu baadae arudi, ni kazi ngumu sana. Lakini magari yangekuja hapa tuna imani kwa asilimia 100 biashara ingefanyika,” ameeleza Mwenyekiti wa soko hilo.