Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla ameitisha kikao kazi na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara kwa lengo la kuweka ustawi msuri wa ufanyaji biashara ikiwa ni pamoja kuweka mazingira bora ili kuinua uchumi wa wafanyabiashara na serikali kupata mapato.
Katika kikao hicho, RC Makalla amepokea changamoto mbalimbali za wafanyabiashara ikiwemo ucheleweshwaji mizigo bandarini, utoaji wa nakala TRA, kamatakamata ya mizigo, idara ya Uhamihaji kutoa muda wa siku saba pekee kwa wafanyabiashara wageni wanaokuja kununua mizigo nchini.
Nyingine ni utaratibu wa Forodha, ushuru wa huduma (service levy) ambapo Jumuiya ya wafanyabiashara wametoa mapendekezo ya kutatua kero hizo.
Kutokana na mapendekezo hayo, RC Makalla ameunda kamati ya kufuatilia na kushughulikiwa kero za wafanyabiashara itakayojumuisha wawakilishi watatu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, wataalamu kutoka mamlaka za udhibiti na usimamizi wa biashara ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Rais Vyombo vya ulinzi na usalama na Kamati itaongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa.
Aidha RC Makalla amesema miongoni mwa mambo kamati itaanza kuyafanyia kazi ni ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyowasilishwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara ambapo pia ameelekeza Wakuu wa Wilaya zote kuhitisha mabaraza ya biashara.
Hata hivyo amesema serikali ya Mkoa huo inaanza mara moja kushughulikia changamoto zilizopo kwenye ngazi ya mkoa na zile zitakazohitaji maamuzi ya mamlaka za juu atawasilisha nakala kwenye ngazi ya Wizara kwaajili ya utekelezaji.
RC Makalla pia ameelekeza TPA kuandika barua kwa TASAC kuzitaka Bandari kavu ICD kuondosha mizigo kwa wakati ili kupunguza changamoto ya mlundikano wa mizigo bandarini.