Home BIASHARA Sababu za mtiririko wa fedha kupungua

Sababu za mtiririko wa fedha kupungua

0 comment 118 views

Mtiririko wa fedha ukiwa mkubwa katika biashara humaanisha kuwa kila kitu kinaenda sawa. Lakini kuna kipindi mambo yanaweza yasiende kama inavyotarajiwa na kupelekea kujiuliza ni wapi unakosea na kusababisha mtiririko wa fedha kupungua katika biashara yako.

Biashara inahitaji kuwa na mzunguko wa fedha ili kumuwezesha mfanyabiashara sio tu kupata faida, bila kuwa katika nafasi ya kufanya mabadiliko kutokana na hali ya soko pamoja na wateja. Unapokosa fedha kwa ajili ya kufanya hayo, inakuwa ngumu kwa biashara kuwapa wateja kila wanachohitaji na kama inavyojulikana, bila wateja hakuna biashara.

Yafuatayo ni mambo ambayo yanaweza kusababisha mtiririko wa fedha kupungua:

Mikopo. Sio vibaya kukopa kwa ajili ya kuendeleza biashara yako lakini mikopo inapokithiri katika biashara lazima mtiririko wako wa fedha uathirike. Hivyo basi, angalia kama una madeni ya kupindukia ili kuweza kuona athari ambazo zinasababishwa wa mikopo hiyo. Pia katika upende mwingine, epuka kukopesha wateja kupita kiasi kwani unapofanya hivyo, unakuwa unatoa bidhaa lakini huingizi fedha.

Cha kufanya: Tengeneza mpango madhubuti ili kuweza kulipa madeni yako, na hakikisha unaepuka madeni yasiyokuwa na umuhimu. Pia hakikisha unajiepusha na madeni kwa ajili ya masuala binafsi na yasiyo na uhusiano na biashara kwa sababu ni ngumu kuzalisha fedha hizo na kuweza kulipa deni.

Pia kuhusu kukopesha wateja: Angalia wateja wenye historia ya kukopa na kutolipa kisha epuka kuendelea kuwakopesha pia jenga utaratibu wa kumkumbusha kila mteja unayemdai ili kulipa mapema. Unaweza kutengeneza sheria ndogo kuhusu ukopaji na ulipaji ili kuendelea kuwa na mawasiliano mazuri na wateja wako kwa kuwa sio wote huwa na nia ya kutolipa madeni yao.

Jambo lingine linaloweza kusababisha mtiririko wa fedha katika biashara kupungua ni tabia ya kununua bidhaa nyingi kuliko mahitaji yaliyopo sokoni. Hali hii inaweza kupelekea bidhaa kukaa sana dukani bila kuuzwa, au kuuzwa lakini kwa bei ya hasara ili kuepusha bidhaa kuharibika kutokana na kukaa kwa muda mrefu.

Cha kufanya: Zingatia muda ambao bidhaa hukaa sokoni na mahitaji ya wateja ili kuweza kutengeneza usawa katika kiasi cha bidhaa na kukidhi mahitaji ya wateja wako bila kupata changamoto ya upungufu wa bidhaa pale wateja wanapohitaji.

Ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kujiwekea utaratibu wa kuandika kila kitu na kuwa na kumbukumbu za kudumu ili kujua mwenendo wa biashara na kufanya mabadiliko pale inapobidi.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter