Home BIASHARA Ukiuzia madini nyumbani tutakufutia leseni: Waziri Mavunde

Ukiuzia madini nyumbani tutakufutia leseni: Waziri Mavunde

0 comment 119 views

Serikali imepiga marufuku biashara ya madini kufanyika majumbani kwa watu na kusisitiza kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili kudhibiti utoroshaji madini na upotevu wa mapato ya Serikali.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema hayo Septemba 17, 2024 Wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo kukagua miradi na maendeleo ya shughuli za madini ambapo ametembelea na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Madini Wilaya ya Tunduru na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushirikiana na wafanyabiashara kufanikisha ujenzi wa soko hilo kubwa lenye kukidhi mahitaji.

Waziri Mavunde ametoa maelekezo ya kuhakikisha biashara yeyote ya madini kufanyika katika eneo moja na rasmi (One Stop Centre) na kwamba Soko hilo lina mifumo bora na miundombinu inayotakiwa kwa mujibu wa Sheria ili kudhibiti na kuziba mianya ya udanganyifu na utoroshaji wa madini kwa manufaa ya taifa na wananchi wake.

“Nitoe maelekezo hapa, ni marufuku biashara yeyote ya madini kufanyika nje ya Soko la Madini, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara ya madini kwa uwazi ili kudhibiti mapato ya Serikali, kukuza sekta, na kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa” amesema Mavunde.

“Tutaleta kikosi kazi (task force) hapa na kufanya operesheni maalum ya kudhibiti na kuwabaini watu wote wanaofanya biashara za kununua madini majumbani ili wakafanye shughuli zao kwenye Soko rasmi la madini, na tutachukua hatua kali za kisheria kwa wote watakao kaidi agizo hili” amesisitiza Mavunde.

Amesema kuwa, kwa mfanyabiashara yeyote atayekamatwa akifanya biashara ya madini majumbani atafutiwa leseni yake, madini hayo yatataifishwa na hataruhusiwa tena kufanya shughuli za madini popote nchini Tanzania.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter