Imeelezwa kuwa, Machi 14 mwaka huu, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajia kufungua soko la dhahabu mkoani Geita. Soko hilo ni la kwanza hapa nchini katika madini ya dhahabu na la tatu kwa ukubwa katika bara la Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema mkoa huo unaongoza katika uzalishaji dhahabu na kwamba, zaidi ya asilimia 40 ya dhahabu yote inayozalishwa Tanzania hutoka mkoani humo.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa mkoa amesema soko kuu la dhahabu litakalokuwa eneo la soko kuu mjini humo litahusisha wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa biashara ya madini wakiwemo wanunuzi, wauzaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, benki na mamlaka ya serikali za mitaa. Gabriel amesisitiza kuwa kuwepo kwa wadau wote katika eneo moja kutaondoa urasimu na kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi.