Home BIASHARA Standard Chartered yatanua wigo wa uwekeaji wa amana kwa wateja wakubwa

Standard Chartered yatanua wigo wa uwekeaji wa amana kwa wateja wakubwa

0 comment 129 views

BENKI ya Standard Chartered jana imezindua huduma mpya ya fedha kwa wateja wake wakubwa, ambao wataweka fedha hizo katika akaunti zao kwa kutumia mashine maalumu (Cash Deposit Machines services-CDMs) zitakazowekwa kwenye eneo la biashara.

Huduma hiyo ni juhudi za benki hiyo kutekeleza matakwa ya wateja wake ya kuwa karibu nao na kurahisisha uwekaji wa fedha na usalama wake.

Huduma hiyo ambayo inawezesha mteja kuwa na mtambo wa kuwekea fedha katika eneo lake la kazi (Cash Deposit Machines services-CDMs) imelenga kwa wafanyabiashara wakubwa kama wenye vituo vya mafuta, maduka makuu, na wauzaji wa vinywaji baridi.

Imeelezwa kuwa CDMs hizo zitafungwa katika maeneo ya biashara hizo na kutoa huduma za kuhifadhi fedha muda wowote ule.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kibenki kwa Makampuni makubwa, ya kati na taasisi za kifedha wa Benki ya Standard Chartered nchini, Bw. James Meitaron (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuzindua mashine maalumu za kuweka fedha (Cash Deposit Machines services-CDMs) kwenye eneo la kazi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma mpya ya fedha kwa wateja wake wakubwa uliofanyika Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa benki hiyo, Bi. Juanita Mramba na kulia ni Meneja Bidhaa wa makampuni makubwa na ya kati wa Benki ya Standard Chartered nchini, Bw. Busara Raymond.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi huo wa huduma za CDMs,  Mkuu wa Kitengo cha huduma za kibenki kwa Mashirika, Biashara na taasisi za kifedha, Bw.  James Meitaron, alisema: “ Benki ya Standard Chartered inazindua Cash Deposit Machines ili kuwezesha wateja wetu wakubwa kuwa na muda zaidi wa kushughulika na kazi na kuacha shaka ya upelekaji wa fedha nyingi kila mara. kwa kuwa na  CDMs wateja wetu sasa wanaweza kuhifadhi fedha katika akaunti zao muda wowote katika mtambo huo. fedha zinazowekwa zitaonesha katika kumbukumbu za kibenki.”

Baadhi ya mashine maalumu za kuweka fedha (Cash Deposit Machines services-CDMs) zitakazowekwa kwenye eneo la kazi kabla ya kuzinduliwa rasmi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.

Aidha alisema kwamba CDMs imeunganishwa na mifumio mingine ya kibenki ya kidigitali ikiwamo Bank’s Corporate Banking Digital platform, S2B, hivyo kumwezesha mteja kuona kinachoendelea katika akaunti yake.

Akizungumzia usalama wa mitambo hiyo, Meitaron alisema kwamba benki inawajibika mara tu fedha hizo zinapowekwa katika mitambo ya CDMs. Pia benki ndiyo itakayosafirisha fedha hizo kutoka katika eneo la mteja hadi benki.

Meneja Bidhaa wa makampuni makubwa na ya kati wa Benki ya Standard Chartered nchini, Bw. Busara Raymond (kulia) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi mashine maalumu ya kuweka fedha (Cash Deposit Machines services-CDMs) kwenye eneo la kazi inavyofanyakazi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma mpya ya fedha kwa wateja wake wakubwa uliofanyika Hoteli ya Hyatt-The Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kibenki kwa Makampuni makubwa, ya kati na taasisi za kifedha wa Benki ya Standard Chartered nchini, Bw. James Meitaron.

Mitambo hiyo itawekwa katika maeneo ya mteja yaliyo salama huku hatua zote za kiusalama zikiwa zimetekelezwa.

Pia mitambo hiyo ina uwezo wa kutambua fedha za bandia na kwamba zitakuwa zinaangaliwa na watu ambao watachaguliwa na wateja wenyewe.

“baadhi ya wateja wetu wana huduma hizi na wameomba mitambo zaidi kutokana na haja  kutunza muda na usalama wa fedha. Nashauri wateja wengi  kujaribu huduma hii watafurahi,” alisema Meitaron

Uzinduzi wa CDMs unafanyika ikiwa ni sehemu ya harakati za benki za kufikia wateja wake pale walipo kwa kutumia njia mbalimbali. Hivi karibuni benki hiyo ilizindua Full Digital Bank on Mobile kwa ajili ya wateja wadogo binafsi na hii ya CDMs ni kwa ajili ya wateja wakubwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter