Home BIASHARA Sukari ya nje yakosa soko

Sukari ya nje yakosa soko

0 comment 139 views

Tani za sukari zipatazo 80000 kati ya 130000 zilizoagizwa na wazalishaji hapa nchini zimekosa soko kutokana na wingi wa sukari inayoingizwa kwa magendo. Sukari hiyo iliagizwa kati ya Machi na Juni mwaka huu kwa lengo la kuziba pengo la mahitaji ya bidhaa hiyo wakati viwanda vya ndani vinaposimamisha uzalishaji.

Mkurugenzi wa Chama cha Wazalishaji wa sukari nchini, Seif Ali Seif ameshauri serikali kuongeza mapambano dhidi ya watu wanaoingiza sukari nchini kinyume cha utaratibu. Seif alisema katika uagizaji wa sukari kuna makundi mawili, wakiwemo wale wanaoagiza kinyume na sheria na wanaoagiza za viwandani na kuziuza kwa matumizi ya nyumbani.

“Sukari ya viwandani ina madhara kwa matumizi ya nyumbani, tukiruhusu sukari hii ikaingia nchini kwetu itasababisha madhara makubwa kwa wananchi. Wananchi watoe ushirikiano kwa  kutoa taarifa waonapo sukari hiyo sokoni” amesema Seif.

Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wanunue vitu vyenye ubora vinavyozalishwa nchini ili kuepuka madhara ya matumizi ya sukari inayoingizwa kimagendo. Ameongeza kwa kusema kuwa, hali ya udhibiti wa sukari kwa sasa inaridhisha baada ya serikali kuingilia kati na kuwapa jukumu wazalishaji kuagiza sukari.

Hata hivyo, amedai kuwa bado wanahitaji jitihada ziongezwe zaidi kwa sababu bado kuna sukari nyingi mitaani.

“Kuna wengine wanaingiza sukari nchini na kuzifunga kwa kutumia vifungashio vinavyofanana na vile vya wazalishaji wa ndani. Tumetembelea baadhi ya maduka na kukuta sukari hizo zinauzwa” Alisema Seif.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa masoko na uendeshaji wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa, Fulgence Bube amesema sukari ya viwandani inapouzwa kwa matumizi ya nyumbani siyo tu ina madhara kwa binadamu, bali pia serikali inakosa mapato. Sukari ya viwandani hutumika kwa ajili mbalimbali ikiwemo kutengeneza vyakula, vinywaji na dawa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter