Home BIASHARA TanTrade, GIZ kuwezesha wafanyabiashara mipakani

TanTrade, GIZ kuwezesha wafanyabiashara mipakani

0 comment 68 views

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Shirika la GIZ zimekubaliana kushirikiana katika uwezeshaji wa Sekta ya biashara hususan kwenye eneo la wafanyabishara wanawake na vijana wanaovuka mipaka.

Aidha, eneo lingine taasisi hizo mbili zimeonesha nia ya kushirikiana ni eneo muhimu la taarifa za biashara na kurahisisha wafanyabiashara kuzipata kwa njia rahisi.
Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Fortunatus Mhambe, ameeleza hayo katika Mkutano uliofanyika kwenye ofisi za TanTrade zilizopo Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K Nyerere, Dar es Salaam.

Amesema uwezeshaji huo unalenga zaidi miradi ya maendeleo kwa wafanyabiashara wajasiriamali wadogo waliopo maeneo ya mipakani ili kuwarahisishia kufanya biashara kwa ufanisi na kukuza biashara zao na uchumi kwa ujumla pamoja na kuwezesha kwenye ukusanyaji wa hatua za uingizaji na uuzaji wa mazao na bidhaa mbalimbali nje ya nchi kwenye Mfumo wa Trade Information Portal.

Meneja wa Mradi kutoka GIZ Bi. Claudia Hofmann amesisitiza kuwa, nchi ya Ujerumani ipo tayari kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Tanzania kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo waliopo mpakani hususan Wanawake na Vijana.

Amebainisha kuwa wamekuja na mpango mkakati wa kuwasaidia wafanyabiashara hao kwa kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zao kwa uhuru na ufanisi zaidi.

“Programu hii inalenga kukuza biashara ndani na nje ya Tanzania hivyo tumejipanga kutoa mafunzo na kuwapa wadau wetu nafasi za kuonesha bidhaa zao, kuwajengea uwezo wa kufanya biashara kwa uhuru na ufanisi zaidi na pia tunatoa nafasi kwa wadau kupata masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi,” amesema Claudia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter